Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Johannesburg
Nipo hapa jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini nikiendelea na mkutano unaojadili uchumi wa vyombo vya habari chini ya taasisi ya CTRL+J.
Mkutano huu unaangalia mwenendo wa mapato, teknolojia ya habari na mitandao ya kijamii vinavyoathiri uchumi wa vyombo vya habari. Si hilo tu, tunaangalia akili unde (AI) inavyozidi kuchanja mbuga na invyoweza kutumiwa kusaidia vyombo vya habari.
Sitanii, pamoja na kwamba nipo hapa Afrika Kusini, moyo wangu upo Tanzania. Ninafuatilia kwa karibu kampeni za Uchaguzi Mkuu na mchakato unavyokwenda.
Nimeona Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilivyopitia mapingamizi 51 yaliyojumuisha ubunge na udiwani. Nimeona Ester Matiko (CCM) alivyombwaga Kangoye Jackson pale Tarime Mjini, huku Ester Bulaya naye akimbwaga kwa pingamizi Pius Masuruli.
Mitandaoni bado ninakiona kilio cha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakitaka Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, aachiwe huru.
Wanasema uchaguzi haunogi bila CHADEMA. Kundi la CHADEMA linaendelea na msimamo wa No Reform, No Election. Lipo pia kundi la Watanzania linalohamasisha watu waende kupiga kura. Kundi hili linaonekana ufuasi wake unaongezeka. Wengi watakwenda kupiga kura.
Vyama vya ACT – Wazalendo na CHAUMA vinaonekana kuwa na nafasi ya nyongeza zamu hii. Tusiyashangae matokeo.
Nimesikiliza kampeni za vyama hivi. Nimeona umati unaofurika. Nimeona mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, anavyovuta ‘nyomi’ kila kona.
Nimeshuhudia mgombea ubunge wa ACT-Wazalendo Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe, anavyojaza wafuasi kwenye mikutano yake ya hadhara. Nimezisikia nyimbo na mbwembwe za wafuasi.
Sitanii, nikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu una ajenda bayana. Kama mwaka 2000 Rais Benjamin Mkapa wa CCM alivyokuwa na ajenda ya elimu akipambana na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, mgombea wa CCM zamu hii ameibua hoja za msingi. Rais Samia ameibua hoja ya gridi ya maji ya taifa. Jambo hili inawezekana halijaeleweka kwa wengi, ila uhalisia ni kuwa mpango huu ni ukombozi.
Kwa miaka mingi, watu wengi nchini wanafanya kilimo cha msimu. Tunajua mahindi, maharage, ufuta, mbaazi, mboga, nyanya, mahindi, mpunga na mazao mengine yote huwa yana msimu wa kuvuna.

Kumbe msimu huu si suala jingine lolote, ni ukosefu wa maji. Ni kutokana na kutegemea kilimo cha mvua. Ndiyo maana Mkoa kama Kagera, hulima mahindi na maharage miezi ya Septemba – Novemba na Januari – Machi (akashaburo) tu.
Hawathubutu kupanda maharage au mahindi katika miezi ya Juni – Agosti (omukyanda). Hali iko hivyo kwa mikoa mingine karibu yote nchini.
Hii maana yake ni kuwa kilimo kinategemea msimu wa mvua. Kwa hii gridi ya taifa ya maji, tunatarajia kuona wakaazi wa Mkoa wa Kagera, hata Karagwe ambayo miezi ya Juni, Julai na Agosti ukiangalia mashamba utadhani yamechomwa moto, sasa wakiwa na kilimo cha umwagiliaji watapanda mahindi na kuvuna katika kipindi cha kiangazi.
Suala hili linaweza kuonekana kama ndoto, lakini lilivyo ni msingi wa kufuta umaskini kwa wakulima. Kuna mikoa kama Dodoma na Singida, kilimo ni msimu mmoja tu. Yaani wakulima wanaingia shambani miezi mitatu kwa mwaka. Miezi tisa ni jua kali, hawana chochote wanachofanya. Kwa kuwa na gridi ya taifa ya maji, hawa watalima angalau miezi 9 katika mwaka, waache mitatu ya mvua za masika.
Ina maana kipato cha watu hawa kitakuwa mara tatu ya kipato chao cha sasa. Maji haya wanapanga kuyachukua kutoka Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na ikibidi Ziwa Nyasa.
Watanzania kama tunavyoona gridi ya umeme uliofika kila kijiji cha Tanzania katika vijiji 12,300, tukiwa na gridi ya maji ya taifa, nchi yetu itaondokana na ukame.
Huu ni msingi mkubwa wa kufuta umaskini, kukuza viwanda vitakavyosindika mazao na kuifanya nchi yetu kuwa ghala la chakula kwa dunia. Mchele unaotoka Thailand unaweza kutoka Tanzania pia.
Nimemsikiliza mgombea Urais wa Chauma, Salum Mwalimu, akiahidi kufufua kahawa na viwanda vya kahawa nchini. Ajenda kama hii ni ya msingi kwa taifa letu. Mgombea wa aina hii, anaonyesha anavyolenga kuwakomboa wakulima wa kahawa nchini.
Ikiwa kikombe cha kahawa kinauzwa kwa karibu Sh 3,000 huko Ulaya, kwa nini sisi tusizalishe kahawa na kusindika kilo moja ikapata bei ya maana?
Kwa upande wao TLP wamesema wakipata urais kila mwanafunzi atasafiri bure. Hii ni hoja mujarabu katika kuboresha mazingira ya elimu nchini. Hii ina maana kila mwanafunzi akisoma katika mazingira yaliyo bora, mwisho wa siku ufaulu utaongezeka na tutakuwa na taifa lenye watoto wenye elimu bora, hali itakayoimarisha ustawi wa taifa letu.
Leo sitazungumzia wagombea wenza. Isipokuwa niseme tu kuwa namsikiliza Mgombea Mwenza wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi. Nasikiliza anavyonadi sera za chama chake. Kwa tunaofahamu protokali, hakika huyu atakuwa Makamu wa Rais kweli.
Akiwa anahutubia mikutano ya hadhara anasema: “Serikali ya Rais Samia… Serikali ya CCM… Rais Samia akishinda… sisi wasaidizi wake tuta…” Lugha hii ni ishara kuwa Dk. Nchimbi anatambua bayana kuwa yeye ni msaidizi wa Rais Samia, si vinginevyo.
Narejea Tanzania wiki hii. Natumaini nitaendelea kufuatilia kampeni zinavyoendelea na katika kipindi hiki nitaendelea kuchambua kwa kina kauli, sera, ahadi na mikutano ya wagombea kuhakikisha kila Mtanzania atakayepiga kura afanye hivyo akiwa na uelewa wa kutosha. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827