Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media,Manyoni

Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kama atapewa ridhaa ya kuwa Rais wa Tanzania kwa awamu nyingine atajenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilayani Manyoni.

Rais Samia ameitoa leo Septemba 9,2025 wakati akiomba kura kwa wananchi wa Manyoni.

Amesema kama atapewa nafasi nyingine anaangalia namna ya kujenga Chuo cha Veta katika eneo hilo ili vijana wengi waweze kujiongezea ujuzi na kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea Serikali.

Aliwashukuru viongozi wa CCM Mkoa wa Dodoma kwa kuratibu na kuandaa vizuri kampeni katika Mkoa huo.

“Nataka nitumie fursa hii kuwashukuru viongozi wote nimemaliza Dodoma leo walikuwa wananifanyia send off na kuja kunisindikiza hapa Singida nawashukuru.Hodi Singida niwashukuru sana kwa bashasha na mapokezi haya,”amesema.

Kuhusu hoja ya kutokuwa na usikivu wa Redio ya Taifa (TBC) Rais Samia amesema kupitia mradi wa uboreshaji watahakikisha wananchi wanapata matangazo ya taarifa mbalimbali zinazorushwa na redio hiyo. Baada ya mkutano huo Rais Samia aliendelea na mkutano mwingine katika eneo la Ikungu.