MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameziagiza wilaya na halmashauri mkoani humo kuhakikisha zinadhibiti matumizi batili ya fedha za mpango wa lishe na badala yake zitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Aidha, amezitaka mamlaka hizo kutoa fedha hizo kwa wakati na kwa kiasi kilichopangwa, bila ucheleweshaji wowote.
Akifunga kikao cha lishe cha mkoa wa Pwani kilichofanyika Septemba 9, 2025, Kunenge alieleza kuwa baadhi ya halmashauri zimekuwa zikitumia fedha hizo kwa shughuli tofauti, jambo ambalo ni kinyume na miongozo ya matumizi ya rasilimali hizo.
“Kwa kufanya hivyo, hamtendi haki. Fedha hizi zinalenga kusaidia jamii, hususan watoto, Huwezi kuwa na Taifa linaloendelea kama wananchi wake hawana afya njema wala lishe bora,” alisema Kunenge.
Aliwataka wataalamu na watendaji wa sekta husika kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ili kuona jinsi masuala ya lishe yanavyopewa kipaumbele na kuhakikisha yanaingizwa katika mipango ya utekelezaji kwenye ngazi zote.
“Tuweke lishe kama ajenda ya msingi. Hakikisheni Mkoa wa Pwani unaendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika utekelezaji wa afua za lishe,” alisisitiza.
Aidha, Kunenge aliwataka wananchi kuendelea kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara, ili kujitambua kiafya na kuchukua hatua stahiki mapema.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, alisema moja ya maeneo muhimu ya kuzingatia ni kuhakikisha afua za lishe zinatengenezwa kwa kuzingatia hali halisi ya jamii, na kuchangia katika uimarishaji wa afya bora.


