Na Cresensia Kapinga, Jamuhuri ,Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amewaongoza viongozi Wadini, Chama na Serikali,wazee na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma katika maombi maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania amani kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kifanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumza katika maombi hayo maalum yaliyofanyika katika ukumbi wa Songea Club mjini Songea, Brig. Jen. Ahmed amesema uchaguzi ni tukio la kidemokrasia lakini wakati mwingine unaweza kuwa ni chanzo cha changamoto nyingi ambazo zinaweza kuharibu Taifa.

“Uchaguzi ni tukio la kidemokrasia lakini pia linaweza kuwa chanzo cha changamoto nyingi ambazo zinaweza kulipalaganyisha Taifa letu, hivyo leo hii tumesimama kama watu wa Mungu kuombea Uchaguzi huu uwe wa amani, haki nahuru, tuombe vyombo vya uchaguzi vifanye kazi kwa weledi na uadilifu, tuombe wagombea wawe na nia njema na moyo wa kushikamana pamoja sio Kwa matusi au rushwa au uchochezi,” alisema Mkuu hiyo wa Mkoa Brigedia Jenerali Ahmed.

Awali akisoma Dua Shekhee wa Wilaya ya Songea Ibrahim Issa alisema kuwa Katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi Taifa linahitaji amani na utulivu kama chaguzi zingine zote zilizowahi kufanyika nchini hivyo ametoa rai kwa watu wote walioshiriki katika maombi hayo maalum kuwa mabalozi wa kuendelea kuhamasisha mshikamano, upendo na umoja na si vinginevyo.