Na WMJJWM – Morogoro

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felista Mdemu amesema dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ahadi zilizotolewa na Tanzania kwenye Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa la mwaka 2021 zinafanikishwa, hususan katika eneo la haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake.

Mdemu ameyasema hayo tarehe 10, Septemba 2025 wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa kilichofanyika katika Ukumbi wa Edema Hotel, mikoani Morogoro.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau kama UNWOMEN na LANDESA itaendelea kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa programu ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanawake, vijana na makundi mengine zinapatiwa majibu ya pamoja.

Aidha, amewataka waratibu kutoka Wizara na Taasisi za umma kuwasilisha taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu utekelezaji wa afua za programu, ikiwemo viashiria na ushahidi wa picha na makala ili kurahisisha maandalizi ya taarifa ya nchi ya miaka mitano.

Mdemu pia amewapongeza wadau wote kwa ushirikiano huku akisisitiza kuwa kazi ya kukuza usawa wa kijinsia haiwezi kufanikishwa kwa Serikali pekee bali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

“Tunapaswa kushirikiana kila mmoja akitimiza jukumu lake, ili kufanikisha ahadi za nchi na kujenga kizazi chenye usawa.” amesema Mdemu.

Pia ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote, huku akisema matarajio ni kuwa kikao hicho kitaibua taarifa thabiti itakayosaidia katika kuboresha utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa kwa miaka ijayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jinsia, Juliana Kibonde amesema kikao hicho kimeandaliwa kwa dhumuni la kupokea taarifa kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali, kujadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha utekelezaji wa programu kwa kipindi kijacho.

Amesisitiza kuwa tathmini kama hiyo ni muhimu ili kuhakikisha Tanzania inabaki kwenye mstari wa mbele katika kusimamia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mwanaamani Mtowo amesema ofisi hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri na Wizara ya Maendeleo ya Jamii katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na mazingira bora na yenye staha mahali pa kazi.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zitaendelezwa kwa karibu ili kuimarisha utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, hususan kwenye eneo la haki na fursa sawa kwa watumishi wa umma.