Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema wafanyakazi wake wataendelea kubakia kwenye Jiji la Gaza licha ya miito ya Jeshi la Israel kuwataka watu wahame kwenye kitovu hicho cha Ukanda wa Gaza.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema juzi kwamba shirika lake limefadhaishwa na amri hiyo ya kuwataka watu milioni moja kwenda kwenye kiitwacho na jeshi la Israel “eneo salama la kibinaadamu ambalo kiuhalisia halipo.”

Mkuu huyo wa WHO alisema nusu ya hospitali zinazoendelea kufanya kwenye Ukanda huo zipo ndani ya Jiji la Gaza na “Ukanda huo hauwezi tena kupoteza vituo zaidi vya afya.”

Msimamo wa WHO ulitolewa wakati jeshi la Israel likiendelea kuyaporomosha majengo makubwa kwenye Jiji hilo, likidai kuharibu vituo vya mawasiliano na mashambulizi vya kundi la Hamas.

Ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, Israel imewauwa Wapalestina 70 kwenye mashambulizi hayo.