Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Nzega
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mratibu wa kampeni za mgombea urais kupitia chama hicho, Bashiru Ally,ametaja sababu tatu za chama hicho kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Amesema chama itaibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu kutokana na mgombea wake kufanya kazi inayoonekana mbele ya Watanzania.

Amezitaja sababu hizo, ni maandalizi kufanyika kwa ufanisi, utekelezaji wa ilani ya CCM, mwitikio wa wananchi, na mvuto wa mgombea Uuais Samia Suluhu Hassa.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Samora leo Septemba 10,2025, Dk. Bashiru amesema mafanikio yanayoonekana ni kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia.
“Kwa maandalizi tuliyonayo, mwitikio mkubwa wa wananchi na utekelezaji wa ilani ya chama, tutashinda kwa kura nyingi. Na baada ya uchaguzi, tathmini itaonyesha kuwa Kanda ya Kati ambayo ni Makao Makuu ya nchi, itaondoka kidedea.
“Nizipongeze Jumuiya ya Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake wa CCM. Hizi ndizo nguzo kuu za ushindi wa chama chetu. Ushindi si jambo la ghafla, ni matokeo ya kazi zao za kila siku,”
Katika hatua nyingine, Bashiru alitoa wito kwa wananchi kutokubali kutishwa kwa maneno au vitendo ili wasishiriki uchaguzi, akisema Serikali ya CCM inalinda haki ya kila mtu aliyejiandikisha kupiga kura kwa amani na utulivu.
“Kutopiga kura kwa sababu ya hofu ni kinyume na haki ya kidemokrasia. Serikali ya CCM inalinda haki hiyo. Kila aliyejiandikisha anatakiwa kushiriki,” aliongeza
Bashiru alisema maandalizi ya uchaguzi mwaka huu yamefanyika kwa ufanisi mkubwa, huku utekelezaji wa ilani ya CCM, mwitikio wa wananchi, na mvuto wa mgombea wao wa urais (Rais Samia) vikitoa ishara njema ya ushindi mkubwa.