Na Mwandishi,JamhuriMedia, Uyui
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema akipewa ridhaa ya kuongoza atafanya kazi kwae kasi ilele.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Ilolanghulu wilayani Uyui mkoani Tabora, leo Septemba 11, Rais Samia hali hiyo inatokana na matarajio makubwa walio nayo wananchi Kwa chama hicho.
“Mkituchagua nawahakikishia tutafanya kazi kwa kasi ileile, wananchi wana matumaini na chama hiki ndiyo chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo.

Amesema wilaya hiyo iliomba watumishi wapya, jambo Hilo limetimizwa.
“Ninafurahi tumeajiri walimu 412 ambao wameletwa ndani ya wilaya hii, watumishi wa afya 161. Tunapoendelea mbele najua bado mahitaji ya watumishi yapo mengi tutayashghulikia.
“Niliahidi ndani ya siku 100 mtakaponipa ridhaa kuendelea kuongoza nchi hii. Ndani ya siku hizo tutaajiri sekta ya afya watumishi 5,000 bila shaka watafika na Uyui,” amesema.
Amesema ndani ya siku hizo, serikali yake itaajiri watumishi 7,000 ambapo wilaya hiyo pia itafikiwa.
Amesema sekta ya afya katika wilaya hiyo serikali imepeleka Sh bilioni 8.2 ambazo zimetumika kujenga vituo vya afya na kuboresha hospitali ya wilaya.
Amesema fedha hizo zimetumika kujenga vituo vya afya sita na zahanati mpya 17, jambo ambalo limepungiza changamoto nyingi.
Pia amesema serikali imepelekq magari matatu ya kuhudumia wagonjwa ambayo yanaendelea kufanyakazi kama ilivyokusudiwa.

“Natambua wilaya hii ni kubwa, mahitaji ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati bado yapo, tupeni nafasi
Kuhusu elimu amesema serikali imeongeza shule saba za sekondari na kufanya idadi kufikia 34 kutoka 27.
Amesema idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 12,000 hadi 17,500, hali ambayo inaonyesha mwamko wa wazazi kupeleka watoto shule.
Amesema serikali imeongeza shule za msingi 28 kutoka 124 hadi 182 na kuendelea kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.
“Tumejenga madarasa ya chekechea. Hii ni programu maalimU ya mwendeleo wa mtoto mapema, tunaweka madarasa haya kwa sababu mama na baba zao hawakuanza shule mapema.
“Walianza kwenda kwenye ng’ombe kwenye shamba lakini sasa tumeanzisha programu ya kumwezesha mtoto aanze shule mapema.”
Alieleza kuwa hiyo ndiyo sababu kwa shule mpya zinazojengwa nchini yanajengwa madarasa ya chekechea ili watoto waanze kukuza akili zao mapema.
Amesema serikali imetekeleza programu za kuimarisha sekta za kilimo na mifugo.
“Tumejenga skimu za umwagiliaji zikiwemo Goweko na Unyanyama na kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu na dawa za chanjo kwa wafugaji.
“Tunapoendelea mbele tutaendelea na ujenzi wa majosho na mabwawa kwa ajili ya mifugo,” alibainisha.
Kuhusu sekta ya maji alisema wilaya hiyo kulikuwa na miradi 15 ambayo imeongeza upatikanaji maji hadi asilimia 67.
Hata hivyo, alisema bado kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajapata maji, lakini kupitia mradi wa Ziwa Viktoria serikali itajenga tanki kubwa la lita milioni moja katika Kata ya Ilolanghulu.
Alisema ujenzi wa tanki hilo litahudumia wananchi wa Ilolanghulu pamoja na kata za Kalola, Isila, Ndono na Mabana.
Pia, alisema ipo miradi ya maji Kigwa, Kizengi na bwawa la Igombe ambayo imefikia hatua mbalimbali za utekelezaji wake.
“Ahadi yangu kwenu ni kuimarisha miradi hiyo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama.
“Mwaka 2022 nilipokuwa hapa mlinieleza kuhusu uhitaji wa daraja la Mto Roya, sasa nataka niwajulishe tumekamilisha usanifu, michoro na gharama ya daraja hilo.
Alisisitiza: “Tumeshatenga fedha ndani ya mwaka huu wa fedha kwa hiyo tunatafuta mkandarasi ili daraja lianze kujengwa. Tutakapojenga tutasaidia wananchi kuvuka kwa raha wakati wa masika.”
Akizungumzia madeni ya wakulima wa tumbaku, alianza kuwapongeza kwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kupitia mbolea na pembejeo za ruzuku wameongeza uzalishaji wa tumbaku hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazouza tumbaku nyingi duniani.
Aliwahakikishia wakulima kwamba serikali bado ipo katika mazungumzo na kampuni za PCL na Volecel ambazo hazijalipa fedha za wakulima.
“Niwahakikishie zitalipwa, kupitia Waziri wa Kilimo huwa ninataka ripoti kila baada ya muda aniambie mazungumzo yamefikia wapi ili wakulima walipwe fedha zao.
Alisisitiza: “Lakini ninafurahi kusema tumeongeza kampuni za kununua tumbaku, sasa kuna ushindani na lile suala la mikopo na wakulima kuchelewa kulipwa fedha zao halipotena.”
Pia, alisema serikali imeendelea kufanyakazi kubwa katika kuhakikisha barabara za vijijini zinaboreshwa kwa kiwango cha changarawe ziweze kupitika mwaka mzima.
Alitaja maeneo ambayo barabara za wilaya hizo zitakwenda kuboreshwa ni Ilolanghulu – Isenga – Kasisi A na Ndono – Fuluma – Makazi.
Alisema katika sekta za maendeleo ya jamii elimu, afya, umeme na maji serikali itakwenda na mwendo uleule.
“Kwa sababu tunajua jinsi watu wetu wanavyokuwa mahitaji yanaongezeka. Katika mahali tutamaliza haja ya umeme tutakapounganisha vitongoji vyote kwa umeme kitakachobaki ni kuunganisha katika nyumba za watu.