Na Ruja Masewa, JamhuriMedia, Mbeya

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na aliyekuwa Spika wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, amemuombea kura mgombea wa urais Samia Suluhu Hassan, kwa Machifu wa Kisafa waliokutanika toka Mbeya Mjini na Mbeya vijijini.

Dk. Tulia alitoa ombi hilo Septemba 11, 2025 baada ya kualikwa na Mkutano wa Machifu ulioandaliwa na Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mbeya na Mjumbe wa Halmashauri ya CCM mkoani humo MNEC Ndele Mwaselele, ulichofanyika ukumbi wa Mkapa Soko Matola, ambapo aliwaomba kura ili kwenye uchaguzi wa Novemba 29, 2025, Chifu Mwenzao (Hangaya) Samia ashinde kwa kishindo.

Mbali ya kumuombea Samia kura, Tulia amewashukuru Machifu hao kwa Mshikamano walioonyesha katika kumkaribisha kwa Bashasha, Mgombea wao wa Urais (Samia) alipohutubia Mbalizi Mbeya hivi katibuni, ili kujinadi na kuomba Kura kwa wananchi, jambo lililomfanya afurahi na kutoa ahadi nyingi mkoani humo, ambapo CCM kikishinda, wao watakuwa na nafasi nzuri ya kufuatilia ahadi hizo.

Aidha Dk. Tulia amewaomba na kuwakumbusha machifu hao kuzisaka kura hizo kwenye kila kata, ambapo wajibu wao mwingine si kuhamasisha tu watu kwenye kaya zao wajitokeze kupiga kura bali baada ya kupiga, pia wanatakiwa kushiriki kulinda kura hizo tangu mwanzo wa kupiga, kuhesabu hadi kutangazwa na kuupokea ushindi huo kwa furaha na amani.

Katika mkutano huo machifu wa Kisafa walimwalika Dk. Tulia kuwa mgeni mwalikwa akiwakilisha Wabunge wenzake wa Mkoa wa Mbeya,na wengine nchini, ambapo kwa niaba yao aliwaombea kura za Chifu mwenzao (Hangaya) Dk. Samia, Wabunge akiwemo yeye (Tulia) na Madiwani wa CCM wa kila kata, kwa wana CCM na wasio wana CCM, ili Novemba 29, 2025 washangilie ushindi wa kishindo.

Machifu hao wakiongozwa na Chifu Mwashinga wamemwahidi Dk Tulia kwamba wanaungana na Chifu Mwenzao Hangaya (Samia) ambaye ndiye kiongozi wao, hivyo wanaahidi kuzisaka Kura, kila kona na watakuwa wa kwanza kupiga kura na baadaye wakawakumbushe na kuwahamisha watu kwenye Kaya zao waenda wakapige Kura kwa Chifu mwenzao Hangaya (Samia Suluhu).

Baada ya mkutano huo, Tulia aliwaaga machifu ambao waliendelea na kikao chao cha kufahamiana, kuwekana sawa na kujenga umoja ili kuelezana mustakabali adilifu wa mila na desturi za Kisafa, ili kuhakikisha zinafanyika kwa weledi.