π Ataja miradi lukuki iliyotekelezwa Bukombe
π Oktoba 29 Katome kumpa kura zote Rais Samia
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema endapo wananchi wa Jimbo hilo watamchagua tena kuwa mbunge wao atahakikisha anafanya jitihada ili wapate maendeleo zaidi ikilinganishwa yale waliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 11, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Katome wilayani Bukombe mkoani Geita, ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

β Nataka niahidi, mkinichagua tena maendeleo tuliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tutazidisha mara mbili kwa miaka mitano ijayo. Tunataka tuibadilishe Bukombe na mnakumbuka tulikuwa na zahanati nne tu wilaya nzima, hatukuwa na jengo la halmshauri na sasa tumejenga majengo yanayofanana na hadhi ya Wilaya ya Bukombe,β amesema Dkt. Biteko.
Akitaja baadhi ya maendeleo iliyofikiwa wilayani humo amesema ina zahanati zaidi ya 60, shule za sekondari za elimu ya upili tano pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na Chuo Kikuu unaoedelea.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Bukombe imebadilika kwa kiasi kikubwa na maendeleo yaliyofikiwa yatazidishwa mara dufu katika miaka mitano ijayo na hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuwachagua wagombea wa CCM.

Kuhusu Kata ya Katome, Dkt. Biteko amesema Kata hiyo haikuwa na mawasiliano ya simu, hospitali, umeme, barabara na shule ya sekondari na iliwalazimu wanafunzi kwenda kusoma Shule ya Sekondari ya Ushirombo.
Aidha, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia ilihakikisha inajenga shule na kuwa na mpango wa kukarabati zilizokuwepo, inajenga zahanati sambamba na kuipandisha hadhi zahanati iliyokuwepo kuwa kituo cha afya ili kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.
Mipango ijayo ya CCM imetajwa kuwa ni pamoja na kujenga barabara ya lami kuunganisha Kata ya Katome na Mbogwe kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na hivyo kuwahakikishia wananchi wakaopisha mradi huo malipo ya fedia
β Mradi wa maji upo tayari tunataka tuupanue zaidi ili maeneo yote watu wapate maji na kazi hii itafanyika mkituchagua, kuna vitongoji sita havina umeme, mkituchagua tena tutaleta umeme kwenye maeneo hayo, tutaongeza minara ya mawasiliano nataka niwaambie mkituchagua tena hamtatudai hayo,βamesema Dkt. Biteko.

Ameongeza βAtakapokuja Rais Samia nataka tumwambie sisi tuko tayari kumpa kura zote, ningependa kuona wapigakura wote 6,500 waliojiandikisha hapa Katome kujitokeza kupiga kura, tunataka tulete maendeleo yanayoonekana si maneno,β
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Katome, Joseph Maganga amesema kuwa CCM imetekeleza miradi mingi ikiwemo kujenga shule za sekondari na miradi ya maji ili kutatua changamoto zilizokuwepo awali.
Hivyo amewahimiza wananchi wa Kata hiyo Oktoba 29 mwaka huu kuwapigia kura wagombea wa CCM.

