Na Kulwa Karedia Jamhuri Media,Kasulu
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuufungua uchumi wa Mkoa wa Kigoma.
Amesema ataimarisha miundombinu ya barabara, kuongeza upatikanaji wa umeme, kuboresha huduma za maji.Samia amesema hayo leo Septemba 13, 2025 mjini Kasulu mkoani Kigoma wakati akiomba kura kwa maelfu ya wananchi wa wilaya hiyo.
Amesema hatua hiyo, itasaidia kuvutia wawekezaji kupitia miradi mbalimbali ikiwamk ile ya kitaifa.
Amesema serikali imejipanga ili kuhakikisha mkoa huo unakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesema kupitia Reli ya Kisasa (SGR) na miradi ya nishati utasaidia kuboresha na kubadili maisha ya wananchi.
“Tunategemea kila kitongoji kinapata umrme ndiyo maana tumeweka hapa shilingi bilioni 58,huku tukikamilisha mradi wa umeme wa maji wa Malagarasi ambao utasaidia kuzalisha megawati 49.5,” amesema.
Amesema umeme kutoka Malagarasi utasambazwa maeneo ya Kidahwe, Buhigwe na Kigoma mjini.
“Hatua hii itarahisisha na kukuza shughuli za uchumi.
Kuhusu miundombinu, Samia amesema serikali itatekeleza miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.

“kwa nia moja tumeamua kujenga barabara zote kwa kiwango cha ndiyo mhimili wa uchumi wa wananchi,” amesema.
Kuhusu huduma za maji, amesema mradi wa miji 28 utaendelea kutekelezwa ili kupunguza tatizo la maji safi na salama
“Tutachimba visima virefu maeneo mbalimbali yenye uhaba mkubwa wa maji,”amesema.
Amesema lengo la serikali ni kuendelea kujenga hospitali na vituo vya afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wote.
Amesema mkoa huo umeanza kunufaika na uwekezaji wa uwapo wa viwanda, kama kile cha saruji na kiwanda cha sukari ambacho kimetoa zaidi ya ajira 500.

“Ukiacha viwanda hivi ipo fursa ya Reli ya kisasa ya SGR na Reli ya zamani hizi zitaifaunya mkoa huu kuwa kitovu cha biashara,”amesema.
Kutokana na hali hiyo, amewaomba wananchi wa hao kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu ili kuchagua CCM Oktoba 29, mwaka huu.
“Mnyonge mimi, naombeni msining’oe. Nawafanyia kazi wanyonge wa Tanzania. Sipendi niwaite sana wanyonge, ila napenda kuwaona wakipata fursa,”amesema.

