Na Kulwa Karedia, Jamhuri Media- Kigoma

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo (CCM), ameunguruma mbele ya mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan.

Akitunia.zaidi ya dakika 11 jukwaani, ameshusha mambo mazito kuhusu Jimbo lake huku akimsifia Rais Samia kwa mafanikio makubwa aliyoiletea nchi.


Amesema serikali yake imefanikiwa kutatua changamoto ambazo kwa muda mrefu zilionekana kuwa mfupa mgumu katika mkoa huo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM leo Septemba 14, 2025 katika uwanja wa Katosho mkoani Kigoma,Baba Levo amekuwa kivitio kutokana na hoja zake nzito alizotoa.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kueleza mambo mazuri yaliyofanhwa na Rais Samia tangu alipoingia madarakani.

Muda wote ambao alitoa hoja na kueleza changamoto za Jimbo lake, alikuwa anashangiliwa na maelfu ya wananchi.
“Umefanya kazi kubwa na nzuri inaonekana machoni mwa wana Kigoma na Watanzania kwa ujumla.

“Miaka yote tuliziita mfupa mgumu kwako zimekuwa biskuti. Mashahidi wa haya ni wananchi wa Kigoma, umegusa maeneo ambayo yalikuwa hajaguswa,”amesema.

Amesema upatikanaji wa maji safi na salama umeboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa miaka minne ya Samia tangu alipoingia madarakani
mwaka 2021.

Kuhusu maji, amesema wanawake walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita mbili kutafuta maji, hali iliyowachosha kimwili na kuwafanya wazeeke kabla ya wakati.Kauli hiyo iliibua shangwe kubwa.

Amesema tatizo la umeme katika mji wa Kigoma limepatiwa ufumbuzi baada ya kuunganishwa na gridi ya Taifa, hatua iliyofanywa baada ya kuzima umeme wa jenereta.

“Tangu nimezaliwa tumekuwa tukihangaika na majenereta. Mama umekuja na kuzima, umetufungamanisha na umeme wa Taifa,leo nasi tunatembea kifua mbele.


Kuhusu maboresho yanayoendelea uwanja wa ndege wa Kigoma, amesema serikali imeonyesha dhamira ya kweli kupeleka wataalamu na vifaa vya ujenzi kuhakikisha eneo hilo linaboreshwa kwa viwango vya kisasa.

“Pale uwanjani tunaona Wachina wanapambana usiku na mchana kuboresha uwanja wetu, wana Kigoma tuseme nini sisi mama,” alihoji.

Ameimba alitumia fursa serikali kutatua changamoto zilizobakia, hasa sekta ya barabara, masoko na fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo

“Mfupa mwingine ni barabara. Vumbi ni tatizo kubwa. Tunaomba barabara ya kilomita 75 ili kurejesha hadhi ya Kigoma Mjini,”amesema.

Aliomba kujengwa soko la kisasa katika Kata ya Kibirizi na kuboreshwa kwa masoko ya jioni ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogo.
Pamoja na mbwembwe zote alimtupia kombora mpinzani Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) kusema ushindi wake uko njia nyeupe.

“Mtu ninaeshindana naye ni dhaifu. Tutampiga saa tano na nusu, tukabidhi asubuhi,”amesema.

Amemuomba Rais Samia kushughulikia kilio cha fidia kwa zaidi ya bilioni 8 kwa wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma ili wawe na furaha wanapoona ndege zikitua na kuruka.