Na Mwandishi Weti, JamhuriMedia, Iringa

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 imelitazama kipekee kundi la vijana kwa kuhakikisha inalijengea mazingira mazuri ya kuliinua kiuchumi.

Amesema moja ya maeneo inayokusudia kuboresha zaidi ili kutoa fursa za kiuchumi ni kupitia sekta ya utalii akitolea mfano mkoa wa Iringa ambako barabara inayokwenda katika Hiifadhi ya Taifa ya Ruaha inajengwa kwa kiwango cha lami ili kucungua kuongeza idadi ya watalii na shughuli za utalii.

Pia, itaboresha zaidi sekta ya kilimo vijana washiriki kwa wingi hatua ambayo itachochea uzalishaji wa ajira za uhakika.

Wasira alieleza hayo kwa nyakati tofauti jana alipohutubia mikutano ya kampeni kuwanadi wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama katika Jimbo la Iringa mjini na Kalenga mkoani Iringa ambapo pia alimuombea kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, jana.

“Tutatengeneza barabara ya kwenda Ruaha (Hifadhi ya Ruaha) vijana wasiokuwa na ajira hapa wataanza kujiajiri kupitia utalii, wanaweza kuanzisha kampuni, wanaweza kukopeshwa watakuwa na magari yanayochukua watalii kwenda Ruaha, na hilo linawezekana kwa sababu vijana wa Arusha na Kilimanjaro ndiyo kazi inayowaweka mjini. Hayo tutayafanya kuleta mapinduzi ya maisha.

“Tunawapa afya, tunawapa elimu lakini wanahitaji fedha mfukoni wanaipataje, unawekeza katika kilimo, unawekeza katika ufugaji, unawekeza katika utalii unafanya watu waishi maisha mazuri,” alisema.

KUBORESHA KILIMO

Alisema kuwa, Mkoa wa Iringa unategemea kilimo kuwa shughulikuu ya uchumi inayotegemewa na wananchi, hivyo serikali itaendelea kuborwsha mazingira kuhakikisha kinafanya vizuri.

“Nyinyi mnalisha Tanzania, mnalima mahindi ambayo siyo kwa ajili ya kula Kalenga pekee, bali kwa ajili ya kulisha Tanzania, kwa hiyo kilimo ni msingi mkubwa wa maisha yetu.

“Chama Cha Mapinduzi kinaahidi kwamba serikali yake itaendelea kutoa ruzuku kwa wakulima na kama mbolea ya ruzuku ilikuwa inachelewa tutaongeza ‘speed’ (kasi) na ufanisi kuhakikisha kwamba inafika kwa wakati na mimi ninayesema na nyie ninaijua habari hii vizuri.

“Nimekuwa waziri wa kilimo maisha yangu yote, ninajua kwa nini mbolea ifike isipofika kwa wakati upande kwa wakati upalie kwa wakati, kama siyo hivyo huwezi kuvuna mwaka mzima, lakini vilevile tunajua kwamba kilimo hakiwezekani kwa kutegemea mvua peke yake kwa sababu kuna matatizo ya tabianchi ambayo yanafanya mvua haijulikani inakuja lini, tunataka kuanzisha vituo vya zana za kilimo vya matrekta wakulima wapate mahala pakukodi kwa gharama nafuu, walime kiangazi na mvua ikinyesha wanapanda,” alisema.

Makamu Mwenyekiti Wasira alisisitiza kuwa CCM lazima ielewe matatizo ya watu iyajibu na kwamba kutokana na ukweli huo ndiyo maana imeleta miradi ya umwagiliaji kutanua fursa ya kilimo kwa wakulima.

Alisema baadhi ya matatizo ya wakulima yanatokana na kutegemea mvua, hivyo katika baadhi ya maeneo mkoani Iringa tumeanzishwa miradi ya umwagiliaji maji kuwa na kilimo cha uhakika.

“Ilani hii inatutuma tuwekeze zaidi katika umwagiliaji kwa sababu wakulima wanataka kuvuna zaidi ya mara moja wavune angalau mara mbili kwa mwaka na tunafanya hivyo makusudi kwa sababu tunajua bado wakulima wetu ni maskini na umaskini wao unatokana na matatizo ya kulima kwa mkono tu wakati wote na kutegemea mvua. Ilani inatutuma kuleta mabadiliko makubwa katika kilimo cha Tanzania.

KUHUSU VIWANDA

Kwa mujibu wa Wasira, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2030 inaelekeza kilimo lazima kiende sambamba na ujenzi wa viwanda.

Alieleza kuwa CCM itaielekeza serikali kuhakikisha kilimo cha mahindi na mazao ya nafaka yapite kiwandani kuyaongeza thamani na kupata fedha nyingi zaidi.

“Nyie mnalima mahindi na mnauza hadi Congo, sasa mnauza mahindi mazima nani anakula mahindi, watu wanataka unga kama ni uji wanywe uji kama ni ugali wapike ugali.
Ilani inatuambia lazima viwanda vitengenezwe na mazao ya wakulima yaongezewe thamani ili mkulima apate bei nzuri kwa sababu ya uhakika wa soko.

“Mazao hayo yaende kwa wale wanaoyataka nje ya Tanzania kama tunauza Kenya tuuze unga kama tunauza Zambia tuuze unga kama tunauza Congo tuuze unga.

“Mazao hayo yakichakatwa mabaki yanayotokana na mahindi yanaweza kutengenezwa chakula cha mifugo kwa hiyo unaoanisha kilimo, mifugo na viwanda. Hiyo ndiyo Ilani ya Chama chetu tunazungumza mambo ya watu hatuzungumzi mambo ya kubabaisha,” alieleza.