Na Jovina Massano, JamhuriMedia, Musoma

WAJASIRIAMALI mkoani Mara waiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanatatua na kusikiliza kero pamoja na changamoto zao kupitia dawati maalum la uwezeshaji lililoanzishwa ili kushiriki kikamilifu katika ulipaji mapato.

Wameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa dawati maalum la uwezeshaji lilozinduliwa na mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi katika viwanja vya TRA Manispaa ya Musoma Septemba 12, 2025.

Uzinduzi huo ni utekelezaji wa mpango mkakati rafiki wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wafanyabiashara hapa nchini kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata uelewa mpana wa umuhimu na wajibu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa na kuendelea kuimarisha sekta ya biashara nchini ambapo Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alilizindua kitaifa Agosti 16, 2025, mkoani Morogoro.

Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara waliofika katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Mara, Charles Waitara amesema dawati hilo liweze kutatua kero na changamoto za wafanyabiashara kwa kuzingatia hatua hiyo italeta majibu kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara.

Ameeleza kuwa miaka ya nyuma wajasiriamali walikuwa wakifukuzana na TRA, lakini sasa hali hiyo haipo kabisa hii inatokana na uwepo wa mahusiano ya Mamlaka na wajasiriamali.

Aidha Waitara amewaomba na kuwasihi wafanyabiashara waendelee kulipa kodi kwa hiari, kwa sababu ndio chanzo Cha Maendeleo popote duniani hakuna nchi inayoendeshwa bila kodi mapato ndiyo msingi wa maendeleo.

Waitara hakusita kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwawezesha Wamachinga kwa kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara na kutoa mkopo wa Shilingi Bilioni 18.5 unaowawezesha kukopeshana na kukuza biashara zao.

Akizindua dawati hilo mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuendeleza ushirikiano na wafanyabiashara pamoja na kuwapa elimu ili kuchochea ufanisi katika shughuli zao, kuimarisha uaminifu, na kukuza uzalendo wa kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya wote na Taifa kwa ujumla.

Kanali Mtambi amewasihi watumishi wa TRA kuendelea kuimarisha mahusiano na sekta binafsi kwa kusogeza huduma kwa wafanyabiashara wasio katika sekta rasmi ili kuwajengea uwezo na kuwapa elimu ya jinsi namna ya kuzirasimisha biashara zao huku akiwahimiza maafisa wa TRA kulitumia dawati hilo kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa sekta rasmi na isiyo rasmi iweze kusaidia kukuza biashara zao.

“Tumieni dawati hili kutatua na kubaini changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa sekta rasmi na isiyo rasmi lengo ni kukuza biashara zao na kuwawezesha kulipa kodi kwa kuwa elimu bora ya kodi na huduma rafiki kwa mlipa kodi ndicho kitawasukuma kulipa kodi kwa hiari”, amesema Mtambi

Kanali Mtambi hakusita kuipongeza TRA Mkoa wa Mara kwa mafanikio katika ukusanyaji wa kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo ukusanyaji ulifanyika kwa ufanisi bila migongano na wafanyabiashara na kuwezesha kuvuka lengo.

Kwa Upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Nasoro Ndemo, ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 walipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 190.1, lakini walivuka lengo kwa kukusanya Shilingi Bilioni 194.62, sawa na ufanisi wa asilimia 102.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliochangia kwa kiasi kikubwa ulipaji kodi wa hiari wa wafanyabiasha.

“Kupitia dawati hili kutawezesha kuwatambua wafanyabiashara kupata taarifa na kusikiliza changamoto zao na kuzitatua Lengo ni kuwasogezea huduma karibu na kuwasaidia kwa kuunganishwa na huduma nyingine, ikiwemo kuwajengea mahusiano na kuwapa elimu ya biashara,” amesema Ndemo.

Nae Joyce Chibwana mfanyabiashara kutoka Kata ya Mwisenge amesema kuwa uwepo wa dawati hilo utawawezesha kufanya biashara katika mazingira bora, ya kirafiki na yenye ushirikiano mzuri na serikali na Mamlaka ya mapato hali itakayowahamasisha kulipa kodi kwa hiari.

Sekta ya biashara hapa nchini, imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa na kuwezesha miradi mbalimbali ya maendeleo kutekelezwa.