Rais Donald Trump wa Marekani amesema yuko tayari kuiwekea vikwazo zaidi Urusi kutokana na vita vya Ukraine lakini ameyataka mataifa ya Ulaya yachukue hatua sawa ya hiyo ya kuitenga zaidi Urusi.
Trump aliwaambia waandishi habari mjini Washington kwamba Ulaya bado inanunua mafuta kutoka Urusi na hata vikwazo ilivyoweka dhidi ya Moscow bado havitoshi.
Aliyataka mataifa ya Ulaya kuacha kununua kabisa nishati ya mafuta ya Urusi na kuunganisha nguvu na Marekani kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi Urusi.
Trump alitoa matamshi hayo katika wakati washirika wake wa Ulaya wanamshinikiza kuichukulia hatua Urusi kutokana na kujivutavuta kwa Moscow kwenye kumaliza vita vya Ukraine.
Mnamo siku za karibuni Trump amekaririwa akisema amevunjwa moyo na Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa kushindwa kwake kuonesha dhamira ya dhati ya kufikia mkataba wa amani na Ukraine licha ya kuahidi kufanya hivyo.
