Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema kufufuliwa kwa Reli ya TAZARA, ujenzi wa reli ya kusini Mtwara -Mbamba bay) utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini.
Amesema ujenzi wa reli hizo amvao upo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030 na kuboreshwa kwa sekta ya kilkmo, kutasaidia kuleta ahueni kubwa ya kiuchumi kwa wakulima hususan wa mkoani Njombe.
Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM kutoka kata 37 zilizo katika majimbo matatu ya Wilaya ya Njombe mkoni Njombe, jana.
“Kwa miaka mitano ijayo Rais Samia (Rais Dk. Samia Suluhu Hassan) amesaini mkataba na China kufufua reli ya TAZARA ambayo inapita Makambako. Reli ya TAZARA itaunganisha maeneo haya na Uwanja wa Ndege wa Songwe na Bandari ya Dar es Salaam na ilikusudiwa hivyo tangu wakati wa Mwalimu Nyerere kwamba tupitishe hii reli kwa sababu kilimo hiki kitaleta mizigo ya kwenda bandarini.
“Pia tunajenga reli nyingine kwa ajili ya watu wa Mtwara kwenda Mbamba bay na tunaunganisha reli kutoka katikati ya Mtwara na Mamba bay kuja Rudewa kwa ajili ya kuchukua chuma cha Liganga na makaa ya mawe ya Nchuchuma, huwezi kubeba chuma kwa lori, lazima tubebe chuma kwa reli tuunganishe Rudewa na bandari ya Mtwara halafu unaiunganisha na duni.
Alieleza kuwa, kwa kufanya maana yake ni kwamba kwa miaka mitano serikali itakayoundwa na CCM italeta mabadiliko makubwa kwa maisha ya wakulima kwa sababu itakuwa imewafikishia mazao yao sokoni kwa urahisi
“Mnalima parachichi, mnalima viazi, mnalima mahindi, mnalima chai, mnalima miti, tena nyie ni wakulima wakubwa wa miti lakini ilani ya Chama chetu inasema ili kuwapa wakulima bei nzuri kwa mazao yao ni lazima kuyaongezea thamani, kwa hiyo tunaoanisha viwanda na kiljmo ili mazao yanayolimwa Njombe yasitoke yalivyo, mahindi mnayolima yasiende Zambia yakiwa mahindi wao wanataka unga tuongeze thamani ya mahindi tuuze unga badala ya kuuza mahindi.
“Tukiyakoboa mabaki ya mahindi yatabaki hapa yatatengemeza chakula cha mifugo na vijana watapata kazi ya kufanya,” alisema.
Alisema Ilani ya Chama Cha Mapindizi inaagiza kuongeza thamani ya mazo, kuanzisha viwanda vinavyochambua mazao yapate mauzo na bei iwe nzuri.
“Kuhusu uchumi, Mkoa wa Niombe ni mkoa wa wakulima na lazima ilani yetu ijibu hoja za wakulima. Tutaendelea kuwapa wakulima huduma za pembejeo kwa ruzuku, tena tunaahidi ruzuku ile iwe inawahi kwa wakati.
“Mimi kazi yangu niliyofanya maisha yangu yote ni kilimo, nilikuwa waziri wa kilimo wa Nyerere, Waziri wa kilimo wa Mwinyi, Waziri wa kilimo wa Kikwete, kilimo tu. Kwa hiyo makamu wa mwenyekiti wa hiki chama ni Bwana Shamba, anajua mambo hayo.
“Na hii Ilani ninayosema nilikuwepo wakati tukiandika, nilikuwa mjumbe wa hii kamati kwa hiyo najua na mawazo yangu yamo humu,” alisema.
Alisema wakulima katika jamii wana umaskini, ingawa kwa mkoa wa Njombe hali siyo mbaya sana kwa sababu wanalima vitu vingi yakiwamo mahindi na viazi hivyo CCM itaendelwa kuwatazama kwa jicho la karibu kuhakikisha inaboresha maisha.
MAENEO MENGINE
Akizungumzia sekta ya afya alisema ilani inaahidi kujenga zahanati 12 katika wilaya ya Njombe kwa miaka mitano kuongeza vituo vya afya vitatu vipya katika miaka mitano ijayo.
Pia itajenga shule za msingi na sekondari zitaongezeka na ujenzi wa Njombe bypass utatekelezwa.
“Tutaendeleza mitaa ya mji wa njombe na mambo mengine mengi ambayo siwezi yote kuyataja yameelezwa kwenye ilani,” alieleza.
