Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze
Mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Mama Salma Kikwete, ametoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze, kumpigia kura za kishindo mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa ni njia pekee ya kuthamini kazi kubwa ya maendeleo aliyotekeleza katika eneo hilo na Taifa.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge Jimbo la Chalinze uliofanyika Uwanja wa Mdaula, Mama Salma alisema Chalinze ni miongoni mwa maeneo yaliyoguswa moja kwa moja na jitihada za Dkt. Samia, hasa katika sekta za afya, elimu, miundombinu na huduma za kijamii.

“Kumchagua Dk. Samia si suala la kisiasa , ni hatua ya kuthamini kazi kubwa aliyoifanya,Kama Chalinze hamtajitokeza kwa wingi kumpigia kura, hamtakuwa mmeitendea haki ,kura zenu ni sauti ya kuthibitisha kuwa mnatambua na kuthamini maendeleo yaliyopatikana,”
Mbali na hilo, Mama Salma alimuombea kura mgombea wa ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia CCM, Ridhiwani Kikwete, akimtaja kuwa ni kiongozi mwenye dira, uzoefu na maono ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.
“Ridhiwani ni kijana wa Chalinze, Mtoto kwa mama hakui, Sisi kama wazazi tuna jukumu la kuhakikisha anapata nafasi ya kuendelea kuwatumikia wananchi wake kwa ari na ufanisi zaidi,” alieleza Mama Salma.
Mama Salma alisema yeye na mumewe, Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, wana imani kubwa na uwezo wa Ridhiwani kuendeleza kazi kubwa aliyoianza, hivyo ni wajibu wao kumsimamia anashinde kwa kishindo.
“Hakuna mzazi ambaye hawezi kusaidia mtoto wake kufanikisha jambo jema, Tunaamini Ridhiwani akipewa nafasi tena, atafanya makubwa zaidi kwa kushirikiana na madiwani wa CCM katika kutekeleza ilani ya chama kwa kipindi cha 2025 hadi 2030,” aliongeza.

Alifafanua kuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete hakuweza kuhudhuria uzinduzi huo kutokana na majukumu ya kitaifa, lakini ametoa salamu kwa wana CCM na wananchi , akiwataka kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi kwa kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.
Vilevile, alieleza kuwa kati ya madiwani 15 wa CCM Jimbo la Chalinze, madiwani 12 tayari wamepita bila kupingwa, jambo linaloonesha imani kubwa kwa chama hicho, na kuwataka wananchi kukamilisha ushindi huo kwa kumpigia kura Ridhiwani Kikwete.
