Jeshi la Israel limeanza operesheni ya ardhini kwenye mji mkubwa zaidi wa Ukanda wa Gaza baada ya majuma kadhaa ya mashambulizi ya anga.

Mtandao wa habari wa Axios umeripoti taarifa hizo ukiwanukuu maafisa kadhaa wa Israeli. Serikali mjini Tel Aviv ilitangaza mpango wa kuukamata mji wa Gaza zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Kwa siku kadhaa sasa jeshi la Israel limekuwa likiushambulia mji huo na kuyaporomosha majengo chungunzima ikiwemo ya ghorofa ikitumia makombora kutokea angani.

Kampeni hiyo ya kijeshi inafanyika licha ya ukosoaji mkubwa wa jumuiya ya kimataifa inayohofia kuushambulia mji wa Gaza kutazidisha madhila yanayowakabili sasa Wapalestina.

Mashirika kadhaa ya kimataifa yamekwishaonya kuwa hali ya kiutu kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina tayari imefikia viwango vya kutisha na operesheni yoyote ya kijeshi itasababisha vifo na maafa zaidi kwa wakaazi wa mji wa Gaza na ukanda mzima.

Mnamo juma lililopita Israel iliongeza shinikizo la kuwataka watu kuondoka Gaza City ikiapa kwamba ni lazima ifanye operesheni kubwa ya kijeshi kuukamata mji huo kwa lengo inalosema kuwa ni kulitokomeza kundi la Hamas.