RAIS wa Marekani Donald Trump amesema Jeshi la Marekani limeharibu meli inayodaiwa kuwa ya mihadarati ya Venezuela iliyokuwa ikisafiri katika bahari ya kimataifa ikielekea Marekani.

Trump alisema siku ya Jumatatu kwamba wanaume watatu waliuawa katika shambulizi dhidi ya “makundi ya ulanguzi wa dawa za kulevya”. Hakutoa ushahidi wowote kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba dawa za kulevya.

Muda mfupi kabla, mwenzake wa Venezuela Nicolás Maduro alisema Caracas itajilinda dhidi ya “uchokozi” wa Marekani, akimtaja mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Marco Rubio “mbabe wa vifo na vita”.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili uliongezeka baada ya Marekani kupeleka meli za kivita kusini mwa Caribbean kwa kile maafisa walisema ni operesheni za kukabiliana na mihadarati, na kufanya shambulizi lililosababisha vifo vya watu 11.