Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora,

Mgombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo amewahakikishia wazee kwamba kwenye Serikali yake wazee wote wenye umri kuanzia miaka 60 watalipwa posho kwa kuwa wameitumikia nchi na wote ni mashujaa.

Mgombea Urais huyo ametoa kauli hiyo alipokuwa wilayani Sikonge Mkoani Tabora kwenye mkutano wake wa hadhara ambapo amesema kwamba misitu yote ya hifadhi ya Tanzania itatumika kulishia mifugo isipokuwa watazuia tu ujenzi wa nyumba.

“Tanzania hii ina wazee wachache karibuni milioni tatu lakini wazee hawa wametelekezwa tunaambiwa hospitalini kuna dawati la wazee lakini nenda sasa hilo kwenye hilo dawati sisi CUF tunasema mtu yeyote mwenye umri kuanzia miaka 60 atalipwa posho kila mwezi kwa kuwa ameitumikia nchi, mmeilisha lakini pia ni mashujaa, “amesisitiza Gombo.

Katika hatua nyingine mgombea urais Gombo amewahakikishia vijana wanaojihusisha na kazi ya bodaboda kuwa watafanya kazi yao kwa amani na uhuru bila kubugudhiwa na mtu.

“Bodaboda mpo… mtakaa kwa amani mtaendesha pikipiki zenu safi kabisa hamtaingiliwa na mtu kwenye serikali ya CUF nyinyi ndio vijana halafu mnaambiwa ndio serikali ya kesho ni Taifa la kesho msijidanganye vijana ni Taifa la leo leo usisubiri kesho leo ndio siku yako, “alisema Gombo.

Kwa upande wake Mgombea mwenza kutoka chama hicho Husna Mohamed Abdallah akiwa kwenye Kijiji cha Kikungu Kata ya Chabutwa Mkoani humo amesema kwamba chama cha cuf kitahakikisha kinaboresha maisha ya watanzania ikiwemo kuongeza ajira, kuongeza uzalishaji wa chakula cha kutosha pamoja na uchumi wa watanzania.