Na Zulfa Mfinanga,JamhuriMedia, Arusha

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendesha mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu pamoja na kuimarisha utawala bora nchini.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanahabari katika kuripoti kwa weledi hasa kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohamed Khamis Hamad, amesema kuwa jukumu la tume si tu kuhamasisha wananchi kutambua haki zao bali pia kuhakikisha taasisi muhimu zikiwemo vyombo vya habari zinatambua wajibu wao katika kulinda demokrasia.

Amesema waandishi wa habari ni miongoni mwa kundi maalum ambalo likipata uelewa wa majukumu yake kisheria na kimaadili itasaidia kuondoa migongano na kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na uwazi.

Akijibu swali lililotokana na tukio la vurugu lililoripotiwa kati ya polisi na wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Tundu Lissu, Hamad alisema tume inalifanyia kazi suala hilo.

“Tumeamua kulifanyia uchunguzi suala hilo ili kujua ukweli wa jambo hilo na tutatoa majibu baada ya uchunguzi wetu kukamilika kwani hata sisi tuna mamlaka ya kufanya uchunguzi,” amesema Hamad.

Aidha amesisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za kitaaluma, kuhakikisha habari wanazoandika au kutangaza zinajikita kwenye ukweli bila upendeleo wa chama, mgombea au msimamo wa kisiasa.

Hamad ameongeza kuwa ni wajibu wa vyombo vya habari kuweka uwiano sawa katika kuripoti shughuli za kampeni za vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi ili kulinda usawa na haki.

Katika mafunzo hayo, waandishi walikumbushwa pia umuhimu wa kutumia mbinu madhubuti za uhakiki wa taarifa (fact checking), hasa katika zama hizi za mitandao ya kijamii ambapo upotoshaji wa habari unasambaa kwa kasi.

Amesema waandishi wanapaswa kuepuka kusambaza taarifa za uongo au kutoa maoni yanayoweza kuchochea chuki, migawanyiko ya kijamii na uvunjifu wa amani badala yake wanapaswa kuwa kiungo cha kudumisha mshikamano wa kitaifa.

Kwa upande wake Afisa Uchunguzi Mkuu wa THBUB, Mohamed Bakary aliwaasa waandishi wa habari kutumia nafasi yao kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.

Alisema ibara ya 21 kifungu cha 1 na 2 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinatoa haki kwa kila raia kupiga kura na pia kuchaguliwa hivyo ni wajibu wa wanahabari kuelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki uchaguzi.

Bakary alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ni msingi wa demokrasia na waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kusukuma mbele ajenda ya uwajibikaji wa viongozi kupitia sanduku la kura.

Aidha ameonya kuwa kuripoti kwa upendeleo au kwa njia inayopotosha kunavunja haki ya wananchi kupata taarifa sahihi na kunaweza kuathiri misingi ya uchaguzi huru na wa haki.

Washiriki wa mafunzo hayo walipata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kazi zao hususan vipindi vya uchaguzi na kupewa mbinu za kuzitatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za kitaaluma.