Na Mwandishi Wetu
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Glory Tausi Shayo, ametembelea Soko la Kawe kufuatia tukio la moto mkubwa ulioteketeza bidhaa na mali za wafanyabiashara wengi wa soko hilo.
Katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 15 Septemba 2025, Bi. Glory shayo alifika katika eneo la tukio na kukutana na Ofisa Mtendaji wa mtaa husika kwa ajili ya kutoa salamu za pole rasmi kwa niaba ya chama na wananchi wa Kawe.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Bi. Shayo alisema:
“Nimetembelea Soko la Kawe lililoungua moto na kuteketeza kwa kiasi kikubwa bidhaa na mali za wafanyabiashara wa soko hilo. Nilifanikiwa kufika kwa Ofisa Mtendaji kutoa pole. Nimeonana na baadhi ya wafanyabiashara mmoja mmoja na kutoa pole za dhati kwa niaba ya wote walioathiriwa na tukio hili la kusikitisha.”

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwafariji waathirika wa tukio hilo na kuhimiza mshikamano miongoni mwa wakazi wa Kawe. Pia alitoa wito kwa jamii:
“Ninawaomba wakazi wote wa Kawe tuungane kwa mshikamano na tushirikiane kuwafariji na kuwasaidia wenzetu waliopoteza mali na riziki zao kufuatia tukio hili.”
Bi. Shayo alibainisha kuwa Soko la Kawe si chanzo tu cha huduma kwa wakazi wa eneo hilo, bali pia ni kitega uchumi muhimu kwa familia nyingi. Ameahidi kuendelea kuwa karibu na wananchi katika kipindi hiki kigumu:

“Hivyo, nipo pamoja nanyi kwa kila hatua wananchi wenzangu wa Kawe katika kipindi hiki kigumu.”
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kutoka eneo la tukio, chanzo halisi cha moto huo bado hakijafahamika, na mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi.
