Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media,Zanzibar

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro, amesema mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, yamejengwa juu ya misingi imara ya falsafa ya R4, ambayo imekuwa dira ya uongozi na maendeleo nchini tangu kuasisiwa kwake

Akielezea kwa kina kuhusu falsafa hiyo ya R4, Dkt. Migiro amesema inahusisha nguzo kuu nne ambazo ni Maridhiano, Mageuzi, Mshikamano na Ustahimilivu.

Amesema falsafa hiyo, si kauli tu ya kisiasa bali ni mtindo wa maisha ambao umeenea ndani na nje ya nchi, na umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya taifa.

Amesema maridhiano yamewezesha kuondoa migawanyiko ya kijamii na kisiasa.

Amesema mageuzi yamefungua milango ya uwekezaji na kuleta ufanisi katika utendaji wa serikali.
Amesema mshikamano umejenga jamii yenye umoja bila tofauti za kisiasa au kijamii, na ustahimilivu umeiwezesha nchi kuvuka changamoto za kiuchumi na kiafya ikiwemo athari za janga la corona.

Amesema Rais Samia ameendeleza dhamira ya mshikamano tangu akiwa Waziri wa Muungano, huku Rais Mwinyi akijipambanua kwa kuimarisha mazingira ya biashara, afya na elimu, hatua ambazo zimewajengea heshima kitaifa na kimataifa.

Amesema kupitia falsafa ya R4, viongozi hao wamewaunganisha Watanzania na kuweka misingi ya maendeleo endelevu.
Aliwataka Watanzania wote kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa tarehe 29, akisisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha usalama na amani vinatawala katika kipindi chote cha uchaguzi.


Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kwenda kuchagua viongozi wa chama kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais .