Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

VIJANA nchini wametakiwa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza amani iliyopo kwa kuwa wao ndiyo kundi kubwa katika jamii na wanabeba mustakabali wa taifa la kesho.

Akizungumza leo Septemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Kongamano la Pili la Ajenda ya Vijana, Amani na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la The African Leadership Initiative for Impact (LII), Joseph Malecela, amesema zaidi ya asilimia 77 ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 35 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, jambo linalothibitisha nafasi yao muhimu katika kulinda na kuimarisha amani.

“Kongamano hili linalofanyika kuanzia Septemba 18 hadi 20 limekusudia kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika ajenda ya amani. Vijana wakiamua kulinda amani, taifa letu litaendelea kuwa na umoja na maendeleo endelevu,” amesema Malecela.

Amefafanua kuwa, longamano hilo linaendana na maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Septemba 21, na limehudhuriwa na vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.

“Mada kuu nne zinatarajiwa kujadiliwa ikiwemo ushiriki wa vijana katika uongozi na michakato ya uamuzi, nafasi ya vijana na amani katika zama za kidigitali, uwezeshaji kiuchumi kama njia ya kuepusha uhalifu, na jitihada za vijana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Malecela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Josephine Matilo, amesema wizara inatambua nafasi kubwa ya vijana na itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha wanapata fursa za ajira ndani na nje ya nchi huku wakipewa elimu juu ya amani na usalama.

“Amani na usalama ni suala linalohusu kila mmoja wetu. Tunawataka vijana waweke kipaumbele katika kulinda amani kwa sababu bila amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana,” amesema Matilo.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema, Taifa haliwezi kuendelea bila uwepo wa vijana hivyo ametoa rai kwa serikali kuhakikisha kunakuwa na mkakati wa kitaifa wa vijana lakini pia kuwahusisha vijana kwenye kufanya maamuzi.

Aidha amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa nyingi kwa vijana katika uongozi mbalimbali wa aerikali na chama lakini pia amewapongeza vijana nchini kwa kutumia fursa mbalimbali za uongozi zinazojitokeza.

“Tunapaswa kuwaleta vijana pamoja na kuwahusisha maswala mbalimbali katika Taifa kwani uwezi ukasema umefanya maendeleo na kuwa na amani na usalama bila kuwahusisha vijana na sio kuwa watazamaji bali wahusishwe kwenye maamuzi,” amesema.

Hata hivyo, Miriam Dominic ambaye ni kijana anaefanya kazi na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Ladies Forum amesema amefurahia kushiriki katika kongamono hilo kama kijana huku akiipongeza serikali kwa kutambua uwepo wa vijana kwa kuwapa nafasi mbalimbali katika uongozi lakini kuweka mikakati kwa ajili ya kuwainua vijana kiuchumi.

“Nimefurahi kuona serikali inatoa fursa za kiuchumi kwa vijana hasa vijana wa kike kwani unapomuinua kijana kiuchumi ni moja ya njia ya kutunza amani nchini kwani atakosa muda wa kukaa kwenye makundi na kupata vishawishi vya uvunjifu wa amani,” amesema.