Na Kulwa Karedia,Jamhuri Media-Zanzibar

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ndiye mgombea sahihi atakayeshirikiana naye kuleta maendeleo.

Amesema ushirikiano huo utaleta manufaa makubwa kwa pande mbili za Muungano.

Rais Samia amesema matokea ya ukuaji uchumi na utekelezaji ahadi za CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeonekana dhahiri uwezo wa kiongozi huyo kuwaongoza vema Wazanzibar.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Septemba 18,2025, Rais Samia amesema maendeleo makubwa yameshuhudiwa Zanziba ikilimganishwa na awamu zingine.

“Pamoja na majanga yote tuliyopitia ikiwemo ugonjwa Covid, tumeweza kufanya kazi kubwa pamoja katika sera za kifedha na uchumi na ndiyo maana hatukuweza kukwamisha miradi yetu.

“Kwenye sera za kifedha na sera za kiuchumi, Dk. Hussein ameweza kusimamia na kuimarisha uchumi ambao kwa sasa unakuwa kwa kasi kubwa,” alisisitiza.

Amesema ukuaji uchumi kwa Tanzania Bara umeongezeka kwa asilimia 6, huku Zanzibar ukiwa juu zaidi kwa asilimia 7.1 kwa mwaka.

“Zaidi uchumi umekuwa hata mifukoni kwa kila mwananchi. Wakati nilipokuwa nikiwasili Nungwi nilikuwa nikitazama kila pande na kujionea namna ambavyo kumejengeka nyumba nzuri za makazi, biashara zinafanyika na mambo yanaenda vyema kwa amani na utulivu,” amesema.

Kuhusu ukuaji wa utalii, Rais Dk. Samia amesema idadi ya watalii imeongezeka ambapo watalii zaidi ya milioni tano wamefika Tanzania Bara, huku zaidi ya watalii 700,000 wamefika visiwani Zanzibar ikiwa ni zaidi ya lengo walilokuwa wamejiwekea.

Kuhusu uchaguzi, Rais Samia amesema chama hicho hakina wasiwasi na ushindi Oktoba 29 mwaka huu kwasababu mambo mengi yamefanyika.

“CCM tunaujasiri kuja kwenu kuomba kura na ujasiri huu unatokana na kufanya mambo makubwa, tunajiamini tutaweza kufanya mambo makubwa.

“Ndiyo maana tunakuja kwenu kwa kujiamini kuomba kura, mtuchague tena ili twende tufanye mambo makubwa zaidi kama alivyosema Dk. Mwinyi,” amesema.

Amesema mambo muhimu yatakayopewa kipaumbele katika kuyatekeleza kwa Watanzania baada ya CCM kupewa ushindi wa kishindo.

Aliyataja mambo hayo ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua maisha ya Watanzania na kuimarisha ustawi wa jamii.
Kulinda amani na utulivu nchini, kudumisha demokrasia na utawala bora na kujenga Taifa linalojitegemea.

Kuhusu suala la kujenga Taifa linalojitegemea, ameswma ili kufikia hatua hiyo ni lazima kila mwananchi hususani vijana awe na shughuli itakayompa kipato.

“Na hii ndiyo kazi inayoendelea kufanywa na CCM ya kuandaa mazingira rafiki kwa vijana kuwa na shughuli za kujishughulisha ili kila mmoja awe na kipato yeye mweyewe asimame ajitegemee na ndiyo kazi tunayoendelea kuifanya.

“Kuweka mazingira kwa vijana wetu kuweza kuwa na shughuli za kujishughulisha kuingiza kipato ili kila mmoja ainue ustawi wa maisha yake na ndiyo tunasema, Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,” alisisitiza Dk. Samia.

Kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Rais Samia amesema kwa kushirikiana na Dk. Mwinyi wameweza kunyanyua maendeleo ya watu kutoka kaya maskini na sasa wana kipato cha kuendesha maisha yao.

Amesema sasa watu wameweza kujitegemea kimaisha,huku akiahidi serikali kuja na awamu nyingine ya mradi huo unaogusa pande zote za Muungano.

Katika mikutano yake iliyofanyika Mkoa wa Kusini Unguja na Kaskazini Unguja imekuwa na mahudhurio makubwa ya wananchi.