Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesema linajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, likitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na usogezeaji wa huduma kwa wananchi, uboreshaji wa maabara, mifumo ya TEHAMA, pamoja na kushiriki kikamilifu katika mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mapema leo Septemba 18,2025 , Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Ashura Katunzi amesema shirika hilo limepiga hatua kubwa katika kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha miundombinu ya sekta za viwanda na biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.
“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, TBS imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yake na kufanikisha matarajio ya wadau pamoja na taifa kwa ujumla,”amesema Katunzi.

Amesema moja ya mafanikio hayo ni ujenzi wa maabara mpya katika mikoa ya kimkakati ya Dodoma na Mwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 36.8 ambapo Dodoma imetengewa zaidi ya bilioni 24.7 na Mwanza zaidi ya bilioni 12.0.
“Maabara ya Dodoma itahudumia mikoa ya Kanda ya Kati ikiwemo Dodoma, Singida na Tabora, huku ya Mwanza ikihudumia mikoa ya Kanda ya Ziwa; Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu,”amesema
Kwa upande mwingine, amesema shirika hilo tayari limepata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kuchora ramani na kusimamia ujenzi wa maabara na ofisi mpya jijini Arusha, ikiwa ni hatua nyingine ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Aidha, amesema TBS imetumia zaidi ya shilingi bilioni 9.8 kuimarisha ofisi zake tisa za kanda ambazo zipo katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita pamoja na maeneo ya mipakani kama Tunduma, Kasumulo, Holili, Namanga, na Bandari ya Mwanza.
“Uboreshaji huu unaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, hasa upimaji wa sampuli za bidhaa, na kuondoa gharama kwa wateja waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma,” ameongeza
Pia amesema TBS imeendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, kurahisisha mawasiliano na kuwezesha utoaji wa huduma kwa njia ya kidigitali, sambamba na kusaidia utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, amesema jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,184 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,359.
“Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya TZS milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote. Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.”amesema
Ameongeza kuwa Shirika limeendelea na huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya bidhaa 8,199 zilisajiliwa na maeneo 47,886 yalisajiliwa
Kwa upande wa mafunzo, amesema TBS imeweza kutoa mafunzo kwa jumla ya wadau 5,437 wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji.

“Mafunzo haya yalihusu dhana nzima ya viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na yamewawezesha kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti ubora,.
Vilevile, amesema TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza u juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora.
Kwa upande Kuongeza Ufanisi wa Maabara amesema TBS ina jumla ya maabara 12 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri, amigo maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya thibati ya umahiri wa kimataifa.
Katika eneo la Kuimarisha Mifumo ya TEHAMA-ICTM alisema Shirika linatumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma zake mbalimbali kama vile leseni ya ubora, ukaguzi wa shehena zinazotoka nje ya nchi na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi, majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji, vyombo vya usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi.
Amesema Mifumo hiyo ni OAS na i-SOMT. Aidha, Shirika limeboresha huduma zake kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini kwa kuunganisha mfumo wake unaoitwa Online Application System na mfumo wa Dirisha TeSWS) ambapo Moja la Huduma (Tanzania electronic Single Window System mfanyabiashara anatuma maombi na anapata huduma za taasisi zote na kibali kupitia mfumo huo.

Vilevile amesema katika Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Serikali katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kutunza mazingira huku ikiokoa maisha kupitia suluhisho endelevu la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kupitia TBS na washirika wa maendeleo na Wizara ya Nishati imeanza kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme vya majumbani.
Vilevile ameongeza kuwa vifaa vya Maabara vya kisasa vinaendelea kununuliwa kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vinavyoingia sokoni vinakidhi viwango vilivyowekwa kabla ya kuwafikia watumiaji. Hatua hii inalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto, kupunguza upotevu wa nishati na hivyo kupunguza gharama watumiaji.
