Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

VIJANA nchini wametakiwa kutambua nafasi yao katika kudumisha amani na usalama, hususan katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.

Wito huo umetolewa leo Septemba 20, 2025 jijini Dar es Salaam na Juma Rashid Ally, Afisa Uwezeshaji Kiuchumi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, wakati wa kufunga Kongamano la Pili la Ajenda ya Vijana, Amani na Usalama.

Amesema vijana wanapaswa kuelewa kuwa amani na usalama ndio chachu ya maendeleo ya Taifa lolote duniani, hivyo hawana budi kushirikiana na Serikali na wadau kuhakikisha misingi hiyo inalindwa na kudumishwa.

“Tukumbuke kuwa tuko kwenye kipindi ambacho tunaelekea Uchaguzi mkuu Oktoba 29, hivyo vijana tunawajibu wa kuhakikisha tunadumisha amani iliyopo. Tusikubali kwa namna yoyote kutumiwa au kutumika katika misingi ya kuvunja amani. Tuangalie mifano katika nchi mbalimbali ambapo kwa sababu za kiuchumi, kijamii au zinginezo wamekosa amani.

“Hatuwezi kupiga hatua bila amani. Taifa letu limejengwa kwa msingi wa mshikamano na kwa asilimia kubwa vijana ndio nguzo kuu. Ili kufanikisha ndoto zetu, jambo la kwanza ni kutanguliza amani na usalama. Hii ni haki na wajibu wetu kama vijana,” amesema.

Aidha, amewakumbusha vijana kutokubali kutumiwa kwa namna yoyote katika kuvunja amani, akisisitiza kuwa ni wajibu wao kuwaenzi waasisi wa Taifa kwa kuendeleza urithi wa mshikamano waliouacha.

Kwa upande wake, Balozi wa Amani, Irene Ishengoma, amesema kuwa kongamano hilo limekuwa sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani, Septemba 21, ambapo vijana walijadili masuala mbalimbali ikiwemo usalama mitandaoni, nafasi za uongozi na maamuzi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kuwawezesha vijana, ikiwemo utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, ambapo vijana hunufaika kwa asilimia 4.

Naye, Sylvia Mkomo, Mwakilishi wa Vijana wa Tanzania katika Kamati shauri ya Umoja wa Afrika kupitia Ofisi ya Vijana ya Umoja huo, amesema vijana wa Tanzania wamepata jukwaa muhimu la ndani la kujadili masuala yao, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo walitegemea mikutano ya nje ya nchi.

“Tunaona sasa Serikali, taasisi zisizo za kiserikali na vijana wenyewe wameonyesha mshikamano mkubwa. Hili linatupa matumaini makubwa kwamba vijana wa Tanzania watakuwa mstari wa mbele katika kuimarisha amani si tu ndani ya nchi, bali pia katika ngazi ya Afrika na dunia,” amesema.