Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuimarisha elimu na maadili nchini, akisisitiza kuwa mchango wao ni nguzo muhimu ya mshikamano na maendeleo ya Taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Septemba 20, 2025 wakati akimuwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Hafla ya Usiku wa Tuzo za Elimu za Mufti, Majaliwa alisema madhehebu ya dini yamekuwa mstari wa mbele si tu katika kufundisha maarifa, bali pia kujenga maadili na uzalendo kwa vijana.

“Serikali ya awamu ya sita inatambua nafasi ya wadau wote wa elimu, ikiwemo BAKWATA na taasisi nyingine za dini, kwa mchango wao katika kuendeleza maarifa, malezi na mshikamano wa kitaifa kupitia elimu,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa elimu haiwezi kuwa kamili bila maadili, kwani maadili ndiyo yanayojenga utu, mshikamano na heshima katika jamii.

Akizungumzia tuzo hizo za Mufti amesema zinatambua ubunifu,uongozi,mshikamano wa jamii na mchango wa wadau katika kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi,bora na endelevu.

“Tuzo za elimu za Mufti ni jukwaa la kitaifa la kutambua na kuthamani mchango wa kipekee katika elimu,ubunifu,malezi na maadili ya vijana wa Kitanzania lakini pia tukio hili linaakisi muonekano wa taifa lenye watu wanaojituma,wanaothamini elimu na wanaochangia ustawi wa Taifa letu bila kukali itikadi za dini au misimamo ya kisiasa”,amesema Majaliwa.

Aidha Majaliwa ameongeza kuwa Baraza Kuu la Kiislam (Bakwata) limekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya elimu nchini kwani limeazisha na kuendesha shule,madrasa na vyuo vinavyotoa elimu bora ya dini na kawaida,sambamba na kujenga maadili mema kwa vijana.

Kwa upande wake, Mufti na Shekhe Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuberi alisema Bakwata imekuwa ikiwekeza katika elimu kwa muda mrefu kwa kuanzisha shule, vyuo na madrasa ambavyo vimezalisha viongozi na wataalamu mbalimbali nchini.

“Tuna watu wengi waliopitia shule za BAKWATA ambao leo hii ni mawaziri, wanasheria, wafanyabiashara wakubwa na viongozi wa umma. Huo ndio uthibitisho wa mchango wetu kwenye elimu ya Taifa,” alisema Mufti.