Ukraine na Urusi zimetupiana lawama baada ya mashambulizi makali kati ya pande hizo mbili usiku wa kuamkia Jumatatu.

Mkuu wa eneo la Crimea lililo chini ya Urusi Sergey Aksyonov amesema watu watatu wameuawa na wengine 16 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya droni ya Ukraine.

Mashambulizi hayo yaliulenga mji wa Foros na kuharibu majengo kadhaa. Urusi imeyalaani na kuyaita mashambulizi hayo kuwa ya kigaidi. Kwa upande wake Ukraine imesema Urusi ilifanya mashambulizi 46 ya anga Jumapili jioni katika mji wa kusini wa Zaporizhzhia na watu watatu wameuawa, wakati idadi ya majeruhi ni watu wawili. Kulingana na kiongozi wa jeshi wa eneo Ivan Fedorov, vikosi vya Urusi vilidondosha mabomu yasiyopungua matano kwenye mji huo.

Hayo yanajiri wakati jeshi la Urusi limesema vikosi vyake sasa vinalidhibiti eneo la Kalynivske, katika mkoa wa Dnipropetrovsk nchini Ukraine.