Na Kulwa Karedia ,JamhuriMedia,Songea
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu ameahidi kufanya mambo makubwa endapo atachaguliwa tena kuongoza nchi.
Rais Samia ametoa kauli Septamba 21,2025 wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Songea kwenye viwanja vya Veta.
Emesema katika sekta za maendeleo ya jamii ambazo ni maji, elimu, afya na umeme serikali zmetekelezwa miradi kasi kubwa.
Amesema sekta ya maji kuna miradi mingi ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya mkoa huo na itakapokamilika itapita kiwango cha upatikanaji maji kilichoelekezwa na ilani ya uchaguzi (2020 – 2025) kama ilivyokuwa imekusudiwa.

“Tunayo miradi inaendelea, maji yatapatikana niwaombe tuwe wastahimilivu ili wakandarasi wafanyekazi zao vizuri na maji yapatikane Kwa wakati,” amesema.
Kuhusu elimu, Rais Samia amesema ujenzi wa madarasa, shule mpya umefanyika huku serikali ikiendelea kutoa elimu bila malipo kuanzia elimu ya msingi mpaka sekondari.
Kwa upande wa ujenzi amesema kazi ya ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha la Songea unaendelea vizuri.
“Ujenzi huu ukikamilika chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 10,000 kwa mkupuo, hii ni habari njema,”amesema.
Amesema sasa fursa nzuri kwa wananchi wa mkoa huo kuhamasika kusoma fani mbalimbali zitakazotolewa chuoni hapo.
Amesema serikali itatekeleza ujenzi wa chuo cha wenyeulemavu eneo la Liganga jimbo la Peramiho kitakachoweza kutoa mafunzo yaliyokusudiwa.

Kuhusu nishati safi, amesema serikali imetekeleza mkakati huo zaidi ya ilivyotarajiwa katika ilani.
“Ilani ilituambia tukifika 2025 vijiji vyote viwe na umeme, tumefanikiwa mno katika hili na serikali ipo katika vitongoji kuunganisha umeme. Karibu nusu ya vitongoji vya Tanzania tayari vimeunganishwa umeme.
“Tunafanya hivi kwa sababu tuliahidi kila wilaya kuwa na kongani za viwanda, tunataka tutakapoanza kuweka kongani za viwanda, umeme uwe umefika,”amesema.
Akitoa mfano Mabada, amesema serikali itaweka viwanda vya kuongeza thamani zao la misitu ili kuongeza ajira na kukuza uchumi kwa vijana.

Amesema uwepo wa umeme kutavutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika maeneo hayo.
Amesema serikali inakusudia kuweka viwanda vya kuongeza thamani zao la kahawa na parachichi.
“Kule Peramiho tumepata mwekezaji mkubwa wa kiwanda cha sukari na shamba kubwa la miwa. Hii pia ni fursa nyingine kutengeneza ajira kwa vijana wetu.
“Mkitupa ridhaa tutaendelea kuwekeza kwa kuongeza tija upatikanaji ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo. Kama mnavyoona matokeo ya ruzuku na pembejeo za kilimo yameongezeka zaidi,” amesema.
Amesema halmashauri ya Songea imeongeza uzalishaji mazao ya chakula kutoka tani 200,000 hadi tani 455,500 kwa mwaka.
Amesema uzalishaji mazao ya kilimo kwa Madaba umepanda kutoka tani 41.7 hadi tani 160,000 kwa mwaka.

Amesema Mbinga, uzalishaji kahawa umepanda na ruzuku ya miche na pembejeo za kilimo zinatolewa na serikali na itaendelea kufanya hivyo.
Amesema uzalishaji kahawa umepanda kutoka tani zaidi ya 100 hadi kufikia tani 300.
Amesema aliwahi kutembelea shamba la mwekezaji ambalo limeajiri watu 3000 hali inayoonyesha mkoa huo kuwa kinara kwa shughuli za kilimo.
“Tutajielekeza kujenga viwanda vya kuongeza thamani ili tuongeze ajira nyingi kwa vijana ndugu zangu,
“Kwa sababu ukiuza unawapa faida wengine wa jirani, mnawapa faida zaidi walime kwao kwa mbolea ya ruzuku, wewe hata ukipata pesa faida zaidi kwa mwenzako,” alisisitiza.
Aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kuchangia vema usalama wa chakula ndani ya nchi na mataifa jirani ambako mahindi yanapelekwa kuuzwa.

Amesema Januari, mwaka huu Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa.
Amesema mkutano huo liliwekwa lengo la ndani ya miaka 10 ijayo (2025 – 2035) asilimia 50 ya kahawa bora inayozalishwa Afrika iwe inasindikwa kabla ya kuuzwa nje ya bara la Afrika.
Amesema hilo ndilo lengo la serikali kutekeleza azimio hilo ambapo CCM imeweka ahadi kuweka mitambo ya kukoboa kahawa kabla haijauzwa.
Amesema serikali imetekeleza mradi wa ujenzi maghala 28 ya kuhifadhia mazao mkoani Ruvuma.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Songea ina maghala 11, Mabada (tisa) Namtumbo (saba) na ghala moja kwa Manispaa ya Songea.
Amesema Manispaa ya Songea serikali itakamilisha ujenzi wa soko la kisasa Manzese A na B.
“Soko hilo ambalo mmelisubiri kwa muda mrefu sasa linajengwa na hatujawasahau wanangu wamachinga mtakuwa na sehemu katika soko hilo.
“Nasema mkoa huu umebarikiwa kuwa na madini mengi kuanzia dhahabu, shaba, makaa ya mawe, madini ujenzi na vito hadi urani yanapatikana ndani ya mkoa huu,” alisisitiza.
Amesema endapo CCM ikipatiwa ridhaa, serikali yake itaanzisha na kuendeleza kongani za viwanda zinazohusiana na madini.
Amesema hatua hiyo, itasaidia kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa huku kipaumbele kikiwa katika uchimbaji na wachimbaji wadogo.

“Tutakwenda kuboresha wachimbaji wadogo lakini pia tutawaelekeza uchimbaji ambao utatunusuru kwenye vifo,” alieleza.
Amesema mwaka huu alifika wilayani Namtumbo kuzindua mradi wa madini ya urani pamoja na kuchimba madini hayo azma ya serikali yachakatwe, yasafirishwe kisha uwepo mtambo wa kuzalisha umeme nchini ili umeme wa uhakika upatikane.
Amesema duniani madini hayo yanakubalika kama nishati safi kwa taifa kuyatumia.
“Tunataka kuufungua mkoa huu wa Ruvuma kuwa kitovu lakini pia ukanda mzima wa kusini (Ruvuma, Mtwara na Lindi) kuwa ukanda wa biashara.
“Kwa maana hiyo mkoa huu tumekamilisha upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege Songea. Nimetua juzi nimeona njia ya kurukia haipungui kilometa tatu inayoruhusu ndege kubwa kutua hapa Songea.
“Njia hiyo ya ndege imeongeza idadi ya miruko ya ndege kutoka 276 hadi miruko 463 kwa mwaka. Na idadi ya abiria 3,971 hadi abiria 20,667 kwa mwaka.”

Amesema awamu ya pili ya marekebisho ya kiwanja hicho ni kujenga jengo la abiria ambalo limefikia asilimia 70.
Amesema jengo hilo litakwenda kuvutia zaidi wasafiri kwa njia ya anga.
Amesema ujenzi wa Bandari ya Mbambabay imefikia asilimia 35.
Amesema serikali imekamilisha ujenzi wa Bandari ya Ndumbi ambayo imechochea biashara baina ya Tanzania na Malawi kupitia Nkatabay hivyo kuongeza fursa za kiuchumi Ziwa Nyasa.
Amesema mwaka jana alizindua barabara ya Mbinga – Mbambabay inayounganisha Bandari ya Mtwara na Mbambabay.
“Tunafungua ukanda ili biashara ziweze kifanyika kwa anga, barabara, maji ili Ruvuma iwe kitovu kikubwa cha biashara.
Tunakwenda kukamilisha barabara ya Kidatu – Ifakara – Malinyi hadi Lumecha inayounganisha Ruvuma na Mkoa wa Morogoro,” alisisitiza.
Aliutaja mradi mwingine ni reli ya viwango vya kisasa ambayo itaunganisha Mtwara hadi Mbambabay.

Amesema serikali ikifanikiwa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 1,000,itaunganisha Mtwara na Ruvuma, kurahisisha usafiri kwa madini yatakayochimbwa Mchuchuma na Liganga.
“Tunafungua ushoroba wa kusini kwa njia zote, anga, maji, barabara na reli ili kuufanya ukanda huu uwe wa kibiashara. amesema licha ya serikali kujenga barabara ya lami kilometa 10 ndani ya mji wa Songea bado msongamano wa magari yapo.
Alikubali ombi la mgombea ubunge wa jimbo la Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro la kujenga barabara ya mchepuko kupunguza msongamano linakwenda kufanyiwakazi.
“Najua bado mna kiu ya barabara na madaraja. Kipaumbele chetu tutakapoendelea ni kukamilisha miradi tuliyoianza alafu ndiyo tutashika ile mingine ambayo tumeianisha kwenye ilani ya uchaguzi.
“Kuna maeneo ambayo mawasilianonya simu siyo mazuri. Hilo nalo tunakwenda kulifanyiakazi kuhakikisha mawasiliano ya simu yawe mazuri kwa sababu ukanda wa biashara lazima uwe na urahisi wa mawasiliano,” alibainisha.
Amesema kuna watu wanazunguka kama yeye wakisema ilani zao, lakini kila nikiwasikiliza ni yaleyale yaliyopo kwenye ilani ya chama chetu lakini ndani ya ilani ya chama cha maoinduzi tukiandika tunajua tutatekeleza kwa njia gani.
Fedha itatoka wapi, vipi tutakamilisha tuliyoyaandika suala siyo kusema tutafanya ndiyo maana tunakuja kwenu kwa ujasiri.