Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha ADA TADEA kimesema kitahakikisha kinatumia maarifa zaidi kufufua kilimo na ufugaji wa kisasa.

Kupitia Ilani yake ya mwaka 2025-2030 kimesema kitaanzisha mashamba makubwa ya ngano kama vile Basotu, mashamba makubwa ya mifugo mfano la Kongwa, Mabuki na mashamba makubwa ya chai, kahawa, pamba, mpunga, alizeti na korosho.

Maboresho hayo yatafanyika pia kufufua na kuanzisha mashamba makubwa ya vitalu vya samaki na mizinga ya nyuki na mashamba

makubwa katika maeneo mbalimbali na kilimo cha mkataba jambo litakalochangia kuwaongezea ujuzi wakulima na wafugaji wadogo na kupata huduma nzuri za ugani na masoko ya uhakika kuinua uchumi wao.

Pia itatoa walau trekta moja kila kata, pawatila moja kila kijiji na plau kwenye eneo la wafugaji.

Serikali yake itatoa ushuru mbalimbali kwa vifaa vyote vya kilimo na kuwafanya wakulima wenye uwezo kununua vitendea kazi vyao.

Pia kimesema serikali yake inaamini kuwa kilimo ni maji hivyo pamoja na mambo yote watatoa kipaumbele kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuhakikisha maeneo yote yanayozunguka maziwa ya Nyasa, Tanganyika, Nyanza, Victoria na Rukwa yanatengenezewa mifumo ya umwagiliaji.

Kimesema ilani hiyo itaondoa ushuru wa vifaa vya kilimo vitakavyotengenezewa mifumo ya umwagiliaji katika mabonde yote likiwamo la Rufiji, Luiche na Mbarali ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji.

Vilevile imeeleza kuwa itafanya juhudi kutufua na kuboresha vituo vyote vya utafiti nchini ikiwamo Ukiriguru, Naliendele, Mlingano, Kilosa, Maruku na Mpwapwa kwa ajili ya utafiti na kuboresha mbegu.

Chama hicho kimesema hali hiyo itaenda sambamba na kufufua na kuboresha ushirika unaotakiwa uwe huru, unaojitegemea kwa mazao yote nchini.