Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mchakato wa Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania ni safari ndefu iliyohusisha maandalizi ya daftari la wapiga kura, uteuzi wa wagombea, kampeni na hatimaye upigaji kura. Kila hatua inabeba uzito wake, lakini kilele cha safari hii ni kura ya mwananchi mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), kila raia mwenye sifa za kuchagua na kuchanguliwa ni mhimili muhimu wa uchaguzi. Hivyo basi, kushiriki kikamilifu si hiari ya kifahari bali ni wajibu wa kiraia.

Sitanii, kampeni ni moyo wa uchaguzi. Wagombea hutumia kipindi hiki kuuza sera na mipango yao ya uongozi. Narudia, ni katika hatua hii, moyo wangu unakuwa mzito. Najiuliza kama tunavyo vyama vya siasa au vikundi vya masilahi.

Inawezekana nisieleweke leo, lakini kesho itakuwa na sura tofauti. Katika dunia hii, kwenye uga wa siasa, uchaguzi ndio mkondo sahihi katika kufikia kila takwa. Kwa yeyote anayetaka kufanya mabadiliko yoyote katika mfumo wa siasa, uchaguzi ndio mpango mzima.

Sitanii, nasema mpango mzima kwa maana kwamba uchaguzi ndio unaompa mtu fursa au chama kuonyesha upungufu wa serikali iliyopo madarakani. Bila kuuma midomo, ndipo hapa nasema, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakikuwatendea haki wafuasi wake na Watanzania walioanza kukiamini kwa kususa uchaguzi. Nitarejea katika hoja hii.

Nafahamu kuwa katika uchaguzi ipo changamoto ya lugha za kejeli, matusi na propaganda zinazolenga kupotosha. Jazba za wanaharakati wanaopotosha ukweli, bila kuchambua hoja na sera kwa umakini katika kipindi cha kampeni ni jambo la kawaida.

Sitanii, katika kipindi cha kampeni utaambiwa Tanzania haina kitu. Utaambiwa tuko nyuma kuliko yeyote awaye. Wanasahau kuwa tunaongoza kama nchi kwa kuwa na treni ndefu ya kisasa ya umeme, ambapo haipo nchi yoyote katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kama sisi.

Wanasahau kuwa katika ukanda huu, ni Tanzania pekee yenye umeme megawati zaidi ya 4,000 na nchi nyingine zinatufuata kwa mbali. Wanasifia Rwanda ambayo mtandao wake wa barabara ina barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,000 tu.

Sitaki kuingia ndani zaidi. Huu ni wakati wa wananchi kuamua kwa vigezo vya uadilifu, uwezo wa kiutendaji na historia ya kiongozi, badala ya kushawishika na maneno matupu. Katika kampeni maneno ni mengi. Tuyachuje.

Sitanii, kura ni silaha isiyo na damu, lakini yenye uwezo wa kubadilisha mustakabali wa taifa. Kupitia kura moja, kiongozi anapewa ridhaa ya kuamua juu ya uchumi, ajira, huduma za jamii na diplomasia ya nchi.

Nasikia hamasa kususia kupiga kura. Kukosa kupiga kura ni sawa na kukabidhi hatima yako kwa uamuzi wa wengine. Kadiri wananchi wanavyoshiriki kwa wingi katika uchaguzi, ndivyo matokeo yanavyokuwa halali na yenye kuakisi matakwa ya wengi. Ikiwa kuna usiyempenda, njia sahihi ni kupiga kura ukamkataa. Si kususa. Hapa ndipo CHADEMA wamekosea. Nipigie.

Kila uchaguzi huibua sauti zinazodai kura haina maana au matokeo yamepangwa. Hizi ni propaganda za kuwavunja moyo wapiga kura. Ukweli ni kwamba, kura ndizo zinazoipa serikali uhalali wa kuongoza. Ukisusa, imeenda hiyo.

Wananchi hawapaswi kukubali kupotoshwa. Badala yake, wachague viongozi kwa kuzingatia sera zenye tija na dhamira ya dhati ya kuwatumikia.

Ikiwa mgombea atasema chama chake kitajenga gridi ya taifa ya maji, kura yako ndiyo ya kuikubali au kuikataa kwa kumchagua unayedhani atatenda yaliyo mema kwa taifa. Tukapige kura.

Sitanii, Watanzania tuelewe kuwa uchaguzi ni fursa ya kuamua mustakabali wa taifa. Kila mmoja wetu ana jukumu la kushiriki kikamilifu. Naamini ulijiandikisha kwenye daftari la wapiga kura. Sikiliza sera za wagombea kwa makini. Piga kura kwa amani na utulivu.

Sitanii, kura yako si ndoto bali ni nguvu halisi. Usiiachie kwa wengine. Siku ya kupiga kura, utoke nyumbani mapema, simama kwenye foleni na upige. Hiyo ndiyo sauti yako na heshima yako. Leo nimeamua nitoe elimu ya mpigakura. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827