Na Kulwa Karedia,Jamhuri Media- Manyara

Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amehitimisha kampeni zake mkoani Manyara, ambapo amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa fedha za ndani na siyo za wafadhili kutoka nje ya nchi.


Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wakati wa mkutano wa kampeni kwenye uwanja stendi ya zamani ya mabasi mjini Babati mkoani Manyara leo Oktoba 4,2025.


Amesema fedha zote zilizotumika ni za ndani kwa mara ya kwanza, jambo ambalo linaonyesha ukomavu wa chama hicho.
“Tumefanya uchaguzi wetu kwa fedha za ndani, hakuna ufadhili,”amesema.


Kuhusu tatizo la magugu maji kwenye maziwa, Rais amesema tayari Serikali imetenga Sh bilioni 1.9 kwa ajili ya kununua mitambo ya kuondoa tatizo hilo katika maziwa mbalimbali nchini.


Amesema ili wananchi wanaendelea kufaidi shughuli za uvuvi, boti nne zitanunuliwa, moja ikiwa ni kwa ajili ya shughuli za ulinzi.
Kwa upande wa sekta ya utalii, amesema serikali ilijiwekea malengo ya kufikisha watalii milioni 5, sawa wamefika milioni 5.3, huku akisistiza miaka mitano ijayo wana lengo la kufikisha watalii milioni 8.


“Natambua Manyara na ukanda wa Kaskazini kwa ujumla ni eneo la utalii, tunategemea kufikisha idadi niliyotaja na hapa kwenu mmenufaika nayo,”amesema.


Amesema serikali imepokea kilio cha wananchi kuhusu wanyama wakali na kwamba tayari hatua za haraka zimechukuliwa.


Amesema imeanzisha vituo vya ulinzi maeneo husika kwa kuweka askari wa wanyamapori wakiwamo wa kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na vijana wa vijijini vya jirani vinavyozunguka hifadhi husika.


“Tumenunua vidani ambavyo wanyama kama tembo wanafungiwa kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wao, wakitoka na kwenda kwenye makazi ya watu, tunatumia ndenge nyuki,”amesema.


Kuhusu sekta ya Madini ameahidi kupima maeneo yote ili kubaini madini yalipo na kuanza kufanya mazungumzo na wawekezaji.
Amesema katika eneo hilo vijana ndiyo wanapewa kipaumbele ili waweze kuwa wazalishaji wakubwa na kupata ajira.