Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewashukuru wananchi wa Misungwi kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wake wa kampeni leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, akisema mwitikio mkubwa ni ishara ya imani kwa chama na viongozi wao.
“Niwashukuruni ninyi wakazi wa Misungwi kwa kujitokeza kwa wingi namna hii… hii Misungwi? Kwahiyo Misungwi hongereni sana. Lakini hii ni imani, imani kwa Chama chenu – Chama Cha Mapinduzi – na imani kwa viongozi wenu,” amesema Dkt. Samia huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Dkt. Samia amesema amerudi Misungwi kwa furaha, takribani miezi minne tu tangu alipohitimisha uzinduzi wa Daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi), ambalo kwa sasa linatumika kikamilifu na limepunguza muda wa usafiri kutoka saa kadhaa hadi dakika chache tu.

Aidha, ameendelea kueleza kwamba miradi yote mikubwa iliyoanzishwa katika Awamu ya Tano wakati akiwa Makamu wa Rais, sasa imekamilika chini ya uongozi wake. Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na reli ya kisasa ya SGR ambayo imefikia asilimia 65 ya ujenzi, na meli ya MV Mwanza ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho za majaribio katika Ziwa Victoria.
DKT. SAMIA AAHIDI KUENDELEZA KILIMO, ELIMU NA NISHATI MISUNGWI
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake ya awamu ya sita imetoa shilingi bilioni 21.6 katika sekta ya elimu mkoani Mwanza katika kipindi cha miaka minne iliyopita, fedha ambazo zimewezesha utekelezaji wa sera ya elimu bila ada, ujenzi wa shule mpya, ongezeko la madarasa na ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA) katika kijiji cha Massawe, wilayani Misungwi.
Akizungumza leo, Jumanne Oktoba 7, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa mnada wa Nyamatala, wilayani Misungwi, Dkt. Samia amesema wilaya hiyo pia imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa kampasi mpya ya Chuo cha Uhasibu, hatua inayolenga kupanua fursa za elimu ya juu kwa vijana wa mkoa huo.
Akiendelea kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Dkt. Samia amesema Serikali yake itaendeleza programu ya ruzuku za mbolea na pembejeo kwa wakulima, sambamba na kutoa chanjo kwa mifugo ili kuimarisha kilimo na ufugaji. Amesema katika kipindi cha miaka minne, mkoa wa Mwanza umenufaika na mgao wa kilo 275,000 za mbegu za pamba na tani 11,050 za mbolea ya ruzuku.

Ameongeza kuwa hatua hizo zimechukuliwa ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji, akisisitiza dhamira ya Serikali kuendeleza kilimo kama sekta kipaumbele katika kukuza uchumi wa wananchi.
Kuhusu sekta ya nishati, Dkt. Samia ameahidi kukamilisha usambazaji wa umeme kwenye vitongoji 323 vilivyosalia wilayani Misungwi, akieleza kuwa hadi sasa vijiji vyote vya jimbo hilo vimepatiwa umeme pamoja na vitongoji 401.
“Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 iliahidi vijiji vyote viwe na umeme, lakini baada ya kufanikisha hilo tumeongeza nguvu hadi vitongoji. Lengo letu ni kila mwananchi mwenye uwezo na mahitaji aweze kupata umeme kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za uzalishaji. Umeme ni maendeleo na usalama wetu,” amesema Dkt. Samia.

DKT. SAMIA: TUTAONGEZA BAJETI YA TARURA KUIMARISHA BARABARA ZA MWANZA
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuboresha mtandao wa barabara Jijini Mwanza na kuhakikisha zinajengwa kwa viwango vinavyokubalika.
Akizungumza leo, Jumanne Oktoba 7, 2025, katika eneo la Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, akiwa kwenye siku yake ya kwanza ya kampeni mkoani humo, Dkt. Samia amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za usafiri na kukuza maendeleo ya kiuchumi katika jiji hilo.
Amefafanua kuwa Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara ya Mwanza City Centre–Buhongwa–Usagara, ambayo itakuwa na njia nne, na kueleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi uko katika hatua za mwisho baada ya tenda kutangazwa.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali pia imepanga kutekeleza ujenzi wa barabara za Mwanza City Centre–Igoma–Kisesa pamoja na Mkuyuni–Maina–Muhangu–Igoma, ambazo tayari zimefanyiwa upembuzi yakinifu na maandalizi ya ujenzi yanaendelea.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, Dkt. Samia amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Buhongwa–Igoma yenye urefu wa kilomita 14 kwa gharama ya shilingi bilioni 22.7, sambamba na madaraja ya Mkuyuni na Mabatini ambayo yamegharimu shilingi bilioni 11.2. Amesisitiza kuwa atahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

