Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mgombea Urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Samandito Gombo, amesema chama chake kimejipanga kikamilifu kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu kwa malengo ya kuleta mabadiliko ya kweli yanayogusa maisha ya kila Mtanzania.

Akizungumza katika mwendelezo wa kampeni zake wiki iliyopita, amesema siasa ya Tanzania inapaswa kuutumikia uchumi wa wananchi na si uchumi kutumikia siasa kama ilivyozoeleka kwa muda mrefu.

“Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakiingia kwenye siasa si kwa ajili ya maendeleo ya taifa bali kwa maslahi binafsi na CUF tumejipanga kujenga taifa lenye maendeleo ya kweli kwa wananchi wote,” amesema.

Gombo amesema CUF itahakikisha haki sawa kwa kila Mtanzania kwa kuweka usawa katika mgao wa rasilimali za taifa na kuondoa dhana kwamba kuna watu wenye haki zaidi ya wengine.

Aidha, amesema wameleta mafanikio katika siasa za Tanzania ikiwamo kupinga kodi ya kichwa iliyofutwa na kusukuma sera ya elimu ya sekondari bila malipo inayotekelezwa japo si kwa kiwango kilichokusudiwa na kupigania miundombinu ya barabara hadi vijijini.

Pia amesema dira ya muda mrefu ya CUF ifikapo mwaka 2030 ni kuijenga Tanzania isiyo na umaskini yenye lishe bora, huduma bora za afya, usawa wa kijinsia na haki kwa wote.

Ameongeza kwa kusema kuwa kwa miaka mingi Watanzania wamekuwa wakiahidiwa maisha bora na CCM lakini hali halisi imekuwa tofauti.

“Badala ya maendeleo tumeshuhudia ongezeko la umasikini, ukosefu wa ajira, ongezeko la rushwa pamoja na ufisadi,” amesema.

Tanzania amesema inahitaji mabadiliko ya kweli na mwanga huo upo ndani ya CUF huku akiahidi kuwa chama chake kimeweka vipaumbele kama kutokomeza umaskini, elimu bora kwa wote na usawa wa kijinsia.

Amesea wataweka vipaumbele kuhakikisha kuwa wanatoa ajira kwa vijana, haki za binadamu pamoja na utawala bora.

“Watanzania wamechoka lakini hawajakata tamaa na huu ndiyo wakati wa mabadiliko ya kweli,” amesema.

Ameahidi kupigania kufutwa kwa sheria ya stakabadhi ghalani inayowanyima wakulima uhuru wa kuuza mazao kwa ushindani wa bei na kutengeneza sheria mpya itakayowanufaisha wakulima moja kwa moja kwa kuimarisha pembejeo na zana za kilimo pamoja na kuweka mpango wa kukabiliana na wanyama waharibifu hasa tembo wanaoshambulia mashamba.

“Tutatumia mfumo wa nyaya za umeme kuzuia tembo kuharibu mashamba ya wananchi kama ilivyofanikiwa Thailand na India,” amesema.

Vilevile amesema kipaumbele chake ni kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji hasa nyakati za masika na kuimarisha huduma za afya kwa wajawazito, watoto na wazee.

Pia ameahidi kupunguza matabaka ya kielimu kati ya wenye nacho na wasionacho huku akisema mshikamano wa kijamii hujengwa kupitia usawa katika elimu.