Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chama cha National League for Democracy (NLD) kimesema serikali yake inawatumia viongozi wa kiroho ili kuhakikisha inakuwa na hofu ya Mungu.
Kauli hiyo imetolewa na mgombea Urais wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, wiki ilyopita wakati akinadi sera zake.
Amesema chama hicho kimekubaliana kitawatumia washauri wa kiroho kutoka katika taasisi za dini kwa ajili ya kumshauri Rais.
“Nikiwa Rais nitaendesha nchi kwa rasilimali zilizopo na si kwa mikopo. Nitatumia madini kama dhahabu, Tanzanite na maliasili zilizopo kuwaongoza Watanzania nikiwa na hofu ya Mungu,” amesema.
Pia amesema wao ndiyo chama pekee cha siasa ilani yake imeona viongozi wa kiroho wawe sehemu ya serikali kwa ajili ya kuwashauri na Oktoba 29, mwaka huu wakichague ili aweze kuongoza nchi iliyonyooka.
“Unapopigwa aya au maandiko unaingia woga kidogo huibi mali ya Watanzania, hivi sasa viongozi wa serikali wamekosa washauri, wamekosa hofu wanabomoa wanavyotaka, nendeni mkanichague niwe rais, katika serikali yangu kukopa ni ni aibu, nakwenda kuongoza serikali isiyokuwa na madeni kwa sababu nchi ina utajiri wa kutosha kuna madini ya kila aina lakini bado hayajawanufaisha Watanzania.
“Wakati kuna nchi kama Saudi Arabia, Libya, Iraq na Qatar wananchi wake hawalipi kodi wanahudumiwa na serikali yao na wao wana mafuta pekee. Wenzetu wanatumia akili gani kunufaika na rasilimali walizokuwa nazo kwa ajili ya raia zao sisi tuna mali wamepewa wazungu, kodi hamuoni inakwenda wapi, maisha ni magumu, Mtanzania leo akiwa tajiri wananchi wenzake wanamsingizia uchawi kwamba huyu atakuwa ni Freemasons ni kwa sababu nchi hai na mfumo wa kuwatengeneza watu kupata utajiri,’’ amesema.
