Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
RAIS wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Kanali Azali Assoumani, ameongoza msafara wa viongozi waandamizi wa Serikali ya Comoro kutembelea Kambi Maalumu ya Matibabu ya Kibingwa inayoendelea katika Hospitali ya Hombo, kisiwani Anjouan.
Katika ziara hiyo ya kihistoria, Rais Azali aliambatana na Dk. Zaidou Youssouf, Gavana wa Kisiwa cha Anjouan; Ahamadi Sidi Nahouda, Waziri wa Afya wa Visiwa vya Comoro; pamoja na Youssoufa Mohamed Ali, Waziri wa Ulinzi, Katibu wa Rais na Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha CRC (Convention pour le Renouveau des Comores).

Ziara hiyo ililenga kutembelea na kuwapongeza madaktari bingwa kutoka Tanzania ambao wamekuwa wakitoa huduma za kibingwa bure kwa wananchi wa Anjouan kupitia uratibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Visiwa vya Comoro.
Katika mapokezi hayo, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Said Yakubu aliwasilisha kwa Rais Azali timu ya madaktari 52 kutoka hospitali kuu tano za taifa la Tanzania Muhimbili National Hospital (MNH), Benjamin Mkapa Hospital (BMH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).
Zingine ni Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) pamoja na Bohari ya Dawa (MSD) na taasisi ya Global Medicare, ambayo ndiyo Mratibu Mkuu wa kambi hiyo.
Baada ya utambulisho wa timu, taasisi zote tano za hospitali, pamoja na MSD na Global Medicare, zilitumia fursa hiyo kutoa zawadi za upendo na kumbukumbu kwa Serikali wa Visiwa vya Comoro.

Zilitoa zawadi hiyo kama ishara ya urafiki, upendo, na ushirikiano wa kudumu katika sekta ya afya. Zawadi hizo zilitolewa kwa heshima kubwa mbele ya Rais Azali, zikionyesha dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana kwa dhati na Comoro katika kuboresha maisha ya wananchi wa pande zote mbili.
Rais Azali Assoumani alipata fursa ya kuwasalimia madaktari hao mmoja mmoja, akionesha upendo na kuthamini mchango wa Tanzania katika sekta ya afya ya Comoro.
Katika hotuba yake fupi, Rais Azali alitoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Balozi wa Tanzania kwa ushirikiano mzuri na Serikali ya Comoro, na akamuomba awasilishe salamu maalumu za pongezi na upendo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa kindugu na wa kibinadamu. Huduma hii si ya kirafiki tu, bali ni ishara ya undugu wa kweli kati ya Comoro na Tanzania. Tumeguswa sana na upendo huu wa dhati,” alisema Rais Azali kwa hisia.
Ziara hiyo imezidisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa juhudi zake katika kusaidia mataifa jirani kupitia diplomasia ya afya na utu.

