Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Kenani Kihongosi, ametoa wito kwa Vijana wote nchini kutokubali kuingizwa mkenge na baadhi ya watu wasio na uzalendo wa Taifa letu wala kujali utu wenye kuendesha magenge ya mitandaoni katika upotoshaji na uhamasishaji wa vurugu zitakazopelekea kuvuruga amani ya nchi yetu na badala yake kusimamia kidete katika kuitunza na kuilinda Amani ya Taifa letu la Tanzania.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwa wingi katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza kwenye muendelezo wa mikutano ya kampeni ya Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Rais Dkt. 𝗦𝗮𝗺𝗶𝗮 𝗦𝘂𝗹𝘂𝗵𝘂 𝗛𝗮𝘀𝘀𝗮𝗻 leo tarehe 8 Oktoba 2025, Mwenezi Kenani amesema watu hao wenye kuhamasisha vurugu si wenye kuishi ndani ya Taifa letu na ni wenye kutumika na walanguzi wenye nia ovu na kutaka kuharibu umoja na mshikamano wetu.

Aidha, Mwenezi Kenani amewataka Vijana na Watanzania kwa ujumla kutokubali kupoteza haki yao ya kikatiba ya kuchagua ama kuchaguliwa ambapo amesema hatua hiyo ni njema zaidi kwa kuanza kushiriki katika mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera na ahadi na baadaye kuwawezesha kuchagua Viongozi wanaoweza kuleta maendeleo na wenye kuwajibika ambapo amesema Viongozi hao wanapatikana ndani ya Chama Cha Mapinduzi pekee kwakuwa ndicho chenye kuhubiri Amani, Umoja, Mshikamano na Maendeleo endelevu.