Umoja wa Mataifa utalazimika kupunguza vikosi vyake vya kulinda amani duniani kote kwa karibu asilimia 25.
Umoja wa Mataifa utalazimika kupunguza vikosi vyake vya kulinda amani duniani kote kwa karibu asilimia 25 kutokana na ukosefu wa fedha, unaohusishwa zaidi na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani.
Hayo ni kwa mujibu wa afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kauli aliyoitoa siku ya Jumatano.
Afisa huyo alisema kwa sharti la kutotajwa jina, kwamba takriban wanajeshi na polisi 13,000 hadi 14,000, pamoja na vifaa vyao, watalazimika kurejeshwa makwao, huku “idadi kubwa ya wafanyikazi wa kiraia katika tume pia ikiathiriwa.
Marekani ilitarajiwa kuchangia dola bilioni 1.3 kati ya jumla ya bajeti ya dola bilioni 5.4 kwa shughuli za ulinzi wa amani za 2025-2026, lakini sasa imeufahamisha Umoja wa Mataifa kwamba italipa karibu nusu tu ya kiasi hicho, au dola milioni 682 — ambazo ni pamoja na dola milioni 85 zilizotengwa kwa ajili ya ujumbe mpya wa kimataifa wa kupambana na magenge na uhallifi nchini Haiti ambao haukuwa katika bajeti ya awali.
China inatarajiwa kuchangia dola bilioni 1.2 katika bajeti ya ulinzi wa amani, ambayo ilikuwa na dola bilioni 2 katika michango ambayo haijalipwa kufikia Julai.
Katika bajeti yake yote, Umoja wa Mataifa sasa unatarajia upungufu wa asilimia 16 hadi 17 katika bajeti ya sasa ya kulinda amani.
