Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amesema kuwa wakati wa kupiga kura Oktoba 29, wananchi wanapaswa kutafakari mambo yaliyoko katika maeneo yao na kuchagua chama chenye uwezo wa kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria, taratibu na ilani za vyama vyao.

Amesema hayo Oktoba 9, 2025, kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, amebainisha kuwa wagombea wa nafasi ya ubunge wameeleza uaminifu wa Dkt. Samia katika kuleta maendeleo nchini, na kwamba yeye mwenyewe akiwa Mwenezi mstaafu ameshuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, afya, kilimo, elimu na miundombinu.

Pia, Makonda amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani, akisisitiza kuwa kura kwa Dkt. Samia ni kura ya maendeleo kutokana na uwezo wake wa kutekeleza ahadi kwa vitendo.

Amesema kuwa Mkoa wa Mara ni mfano wa mafanikio ya wanawake ndani ya CCM, kwa kuwa umepata wagombea ubunge wanne wanawake kupitia kura za maoni na vikao vya chama, jambo linaloonesha uongozi thabiti wa Dkt. Samia kama mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM  katika kuwaamini wanawake.