Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, leo Oktoba 9, 2025, amezindua rasmi programu ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme”, ubunifu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) unaolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Programu hiyo, iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam, inalenga kuhamasisha wananchi kutumia umeme kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa gharama nafuu, ufanisi mkubwa na matumizi madogo ya umeme ikilinganishwa na nishati nyingine.

Akizungumza katika uzinduzi huo, RC Chalamila ameipongeza Wizara ya Nishati, TANESCO, na wadau wa maendeleo kwa ubunifu huo, akisema ni hatua muhimu katika kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi na endelevu.
“Mpango huu ni mwanzo wa zama mpya katika historia ya huduma za umeme nchini. Unaunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu katika matumizi ya nishati safi na unaonyesha dhamira ya serikali kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa matumizi ya umeme kwa shughuli za nyumbani, ikiwemo upishi, ni msingi wa kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa nishati (Energy Compact) ambao unalenga kuunganisha wateja milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030, sawa na wateja wapya milioni 1.7 kila mwaka.
“Kupitia mpango huu, mteja ataweza kupewa jiko wakati wa kuunganishiwa umeme na atalipa kidogo kidogo kupitia mfumo wa token. Hii itarahisisha familia nyingi kupika kwa ufanisi na kwa gharama nafuu,” ameeleza Twange.
Katika hatua nyingine, RC Chalamila pia aligawa majiko ya nishati safi kwa wananchi waliokuwa wakihudhuria hafla hiyo na kuwataka kuwa mabalozi wa matumizi ya umeme kupikia katika jamii zao.



