Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Kagera
Mgombea udiwani kupitia tiketi ya ACT WAZALENDO kata Mabale jimbo la Misenyi mkoani Kagera Mhandisi Sweetberty Kaizilege Jonh amewaahidi bima ya afya kundi la wazee na wajane ili kuwasadia kupata matibabu bure.
Mgombea Sweetberty ameyabainisha hayo wakati akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni zilizofanyika senta ya Nfatila kitongoji Kiumulo kijiji Kibeo ambapo amesema kwamba kundi la wazee na wajane limekuwa likizipitia changamoto dhidi ya upatikanaji wa matibabu kutokana na hali duni ya kipato hivyo iwapo atachaguliwa kuwa diwani atahakikisha wananchi wa makundi hayo wananufaika na bima ili kuwaondolea adha hiyo.

Sambamba na hilo amesikitishwa na kitendo cha akina mama kushiriki shughuli za uandaaji kokoto milimani zinazotumika katika ujenzi wa zahanati ya kijiji ambayo iko hatua ya msingi baada ya mama mmoja Adelina Runyiga kujitokeza mbele ya mkutano na kuelezea kero hiyo akisema kwamba akina mama wamekuwa wakishirikishwa zoezi la kujitolea juu ya ujenzi wa zahanati hususani kazi ya kuandaa na kubeba kokoto kichwani jambo ambalo limekuwa chungu kwao hivyo wamemuahidi mgombea kumpatia kura za kishindo ili aweze kuwanusuru na kadhia hiyo.
Mgombea huyo amewaahidi akina mama hao kuwa watakapompatia ridhaa changamoto hiyo haitakuwepo tena kwani haileti taswira nzuri kwa akina mama kupambana na mawe milimani badala yake utawekwa mpango thabiti utakaowezesha kufanikiwa ujenzi wa zahanati hiyo ili wananchi waweze kunufaika na huduma bora za afya.
Hata hivyo amesisitiza kuwa dhamira yake ni kutatua changamoto za wananchi hususani maji na barabara kutokana na maeneo mengi ya kata ya Mabale kukabiliwa na changamoto hizo pamoja na suala la kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja ili kuwawezesha wananchi makundi yote vijana, akina mama na wazee kuongeza kiwango cha mapato yao.

Naye katibu wa ACT jimbo la Misenyi Lauliani Kabakama akiendelea kuwanadi wagombea maeneo mbalimbali amewaeleza wananchi wa Kiumulo kuwa chama hicho kimewateua wagombea bora watakaowasaidia kuwaletea maendeleo hivyo amewasihi Oktoba 29 mwaka huu wa 2025 wananchi waliojiandikisha kujitokeza na kupiga kura kwa wagombea wa ACT WAZALENDO ili waweze kuwatumikia na kuwaletea maendeleo kwa kasi.




