Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kamati ya Vibali vya Ujenzi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake kwa kufanya ukaguzi wa kustukiza katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Gerezani, Kariakoo, ambapo imebaini kasoro kadhaa kwenye baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa.
Katika ukaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, kamati hiyo ilitembelea maeneo tofauti tofauti ndani ya kata hiyo na kugundua mapungufu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa vibali halali vya ujenzi, michoro ya majengo pamoja na nyaraka muhimu za ukaguzi.

Kutokana na hali hiyo, kamati ililazimika kutoa maagizo ya kusimamisha ujenzi katika baadhi ya maeneo hayo hadi wamiliki watakapowasilisha nyaraka zinazohitajika.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Vibali vya Ujenzi wa Jiji la Dar es Salaam,laurean Revelian, amesema kamati hiyo ni mpya na imejipanga kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inatekelezwa jiji inazingatia sheria na kanuni za ujenzi.
“Tumeanza na Kata ya Gerezani kama sehemu ya mkakati wetu wa kufanya ukaguzi wa kustukiza katika jiji lote,lengo ni kuhakikisha kila jengo linalojengwa linafuata taratibu za kisheria ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na ujenzi holela,” amesema.

Akifafanua kuwa kamati hiyo haitakuwa na ratiba maalum ya ukaguzi, bali itakuwa ikitembelea maeneo mbalimbali kwa ghafla ili kubaini changamoto zinazojitokeza katika shughuli za ujenzi.
“Katika maeneo tuliyotembelea, hatukukuta wahandisi wakisimamia kazi, hali inayodhihirisha kuwa baadhi yao wanawaachia (sub contactor )mafundi wa kawaida kuendeleza ujenzi bila uangalizi wa kitaalamu hili ni jambo hatari kwa usalama wa majengo na watu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Levelian, kamati imeweka notisi katika maeneo yaliyobainika kuwa na mapungufu na kuwataka wamiliki wa majengo kufika ofisini kwao wakiwa na vibali, michoro na nyaraka nyingine muhimu kabla ya kuendelea na shughuli za ujenzi.
Aidha amesema endapo watashindwa kufanya hivyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa watakaopuuza wito wa stop oda walizoweka kwenye maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Valelian Mombuli, ambaye alishiriki katika ukaguzi huo, amesema majengo mengi hayajazingatia kanuni za usalama wa moto na uokoaji.
“Tumeona baadhi ya majengo hayana mifumo ya kuzima moto, njia za dharura wala vifaa vya usalama kama ‘fire control panels kwani sheria zipo wazi lakini utekelezaji wake bado ni hafifu,” amesema .
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaoomba vibali vya ujenzi kufuata ushauri wa wataalamu wa ujenzi na kuhakikisha majengo yao yana miundombinu ya usalama wakati wa kufanya ujenzi ili kuepusha hatari.
“Kila jengo linapaswa kuwa na ngazi za kawaida na za dharura kulingana na ukubwa wake kama haya yote tuliotembelea yalipaswa kuwa na njia mbili kwa hiyo ni muhimu kuzingatia ushauri huu ili kuepusha majanga kama moto au maafa mengine,” ameongeza.
Kamati hiyo imesisitiza kuwa ukaguzi wa kustukiza utaendelea katika kata nyingine zote za jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kudhibiti ujenzi holela na kulinda usalama wa wakazi wa jiji .

