Na Mwandishi Wetu Jamhuri Media,Mbogwe

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali imeanzisha Mkoa wa Kimadini wilayani Mbogwe ili kufikisha huduma kwa wachimbaji haraka.


Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Mbogwe mkoani Geita wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu leo Oktoba 12,2025, Rais Samia amesema hana wasiwasi wa wananchi wa wilaya hiyo kutokana na kukubalika kwake.


“Hapa Mbogwe mambo mengi yamefanyika kama alivyosema mwenyekiti hii ni wilaya yenye fedha, amani, furaha na utajiri mkubwa, nawashukuru sana,”amesema.


Amesema kutokana na umuhimu wa kutambua shughuli za madini, Serikali ilianzisha Mkoa wa Kimadini ili kusogeza huduma kwa wachimbaji.


Amesema kutokana na kuwajali na kuthamini mchango wa madini, Serikali imejipanga kufanya utafiti mkubwa wa maeneo yenye madini.


Amesema mpaka sasa Serikali imepima asilimia 16 tu ya nchi na mpango wake mkubwa ni kupima asilimia 18 ili kubaini maeneo zaidi.


“Kipaumbele chetu ni kupima asilimia 18 ili kubaini madini zaidi, hii ni fursa kubwa kwa vijana wetu ambao ndiyo wanaotakiwa kutumia rasimali hii kwa ustawi wetu,”amesema.


Kuhusu huduma ya maji, Rais Samia amesema Wilaya ya Mbogwe imepiga mesema hatua kubwa ya upatikanaji maji ambapo sasa imefikia asilimia 86 tofauti na miaka ya nyuma.


“Najua kuna kata chache ambazo zinakabiliwa na uhaba wa maji hasa kipindi hiki cha kiangazi, napenda kuwambia tayari tuna mradi wa shilingu bilioni 4 ambazo zipo kwenye mradi wa Masumbwe ambao umefikia asilimia 68 kukamilika.


“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunakamilisha mradi huu Kwa wakati ili kila mwananchi wa Mbogwe apate maji,”amesema.


Kuhusu afya, Rais Samia amesema wamefanya maboresho makubwa katika hospitali ya wilaya kwa sababu lengo la Serikali ni kila mwananchi apete huduma karibu na eneo analoishi.


Amewaahidi wananchi wa wilaya hiyo kama wakimpa ridhaa tena, Serikali itajenga soko la kisasa na maghala ya kuhifadhia chakula
Amesema kuna mahitaji ya barabara ikiwamo ya Masumbwe yenye urefu wa kilomita 45 itajengwa kwa kiwango cha lami.


Kuhusu elimu,afya, umeme na barabara, amesema hiyo ni shughuli endelevu kwa sababu ni maendeleo ya jamii ambayo kila wakati lazima yashughulikiwe.


“Nawaahidi Serikali ya CCM iko mbele yenu hapa, tupeni kazi tukaifanye kazi miaka mitano ijayo ili tuimarishe utu wa kila mtu ndiyo maana kauli mbiu yetu ni “Kazi na Utu tunasonga mbele”