Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Mgombea Urais kupitia chama cha wananchi (CUF) Gombo Samandito amesema endapo wananchi wakimpa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ataondoa utitiri wa kodi nchini ambapo ataweka mfumo mmoja wa ukusanyaji kodi kupitia kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kuondoa mianya ya rushwa kwa mamlaka ya mapato Tanzania ( TRA).
Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Ruvuma (RPC) wakati wa kusaka kura za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu ambapo atahutubia wakazi wa manispaa ya Songea katika viwanja vya greenbelt vilivyopo mtaa wa Ruvuma kata ya Ruvuma kwenye manispaa hiyo.

Alisema kuwa mfumo mmoja wa ukusanyaji kodi kupitia NIDA unalenga kuleta uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ambapo utalenga kuunganisha utambulisho wa mtu binafsi na taarifa zake za kifedha.
” Mpango huu wa kutumia NIDA katika ukusanyaji wa kodi utakuwa mwepesi katika kufuatilia mapato na ushuru kwa usahihi ,utapunguza mianya ya ukwepaji kodi, kupunguza utegemezi kwa mifumo mingi inayojirudia lakini kubwa zaidi kuongeza uwajibikaji wa walipa kodi na Taasisi za ukusanyaji”alisema Samandito.
Aidha alisema kuwa akiingia madarakani ataanza na bajeti ya trioni 200 ambayo itatosha kuhudumia wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu bure kama huduma za afya, elimu,maji,umeme vyote vitatolewa bure hakuna haja ya kuwatoza wananchi fedha nchi inautajiri mkubwa.
Amewataka wananchi ili haya aliyoyasema yaweze kutimia amewaomba wajitokezekwa wingi kwenda kumpigia kura za kishindo mgombea wa CUF kupitia kiti cha Urais pamoja na mgombea mwenza wachama hicho nakwamba wananchi wasiogope hakuna vurugu zozote zitakazo jitokeza Oktoba 29 mwaka huu.