Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea na kampeni zake leo mkoani Geita kwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika maeneo ya Mbogwe, Bukombe na Runzewe.
Katika mikutano hiyo, Dkt. Samia amewataka wananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi, kushikamana na kudumisha umoja kama silaha muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu. Amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ni matokeo ya uongozi wa serikali thabiti yenye maono na inayojali wananchi wake.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika mkoa wa Geita, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, kuboresha huduma za afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na salama vijijini.
“Maendeleo haya tunayoyaona leo siyo ya bahati mbaya, ni matokeo ya amani tuliyoilinda kwa muda mrefu na uongozi makini wa CCM unaosikiliza wananchi wake,” alisema Dkt. Samia huku wananchi wakimshangilia kwa hamasa kubwa.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Geita kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, kupiga kura kwa amani na kisha kurejea majumbani kusubiri matokeo kwa utulivu, akisisitiza kuwa uchaguzi ni sehemu ya demokrasia inayojenga taifa.
Kampeni za Dkt. Samia zinaendelea leo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita, ambapo anazungumza moja kwa moja na wananchi kuhusu dira ya maendeleo ya CCM kwa miaka mitano ijayo.
