Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameahidi kujenga kituo cha kukuza vipaji na michezo katika eneo la Sokoine, Ipala ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuendeleza vijana na kuhamasisha uwekezaji katika Kata ya Ipala.

Akizungumza wakati wa mwendelezo wa mikutano ya kampeni zake iliyofanyika katika kata hiyo jana, amesema wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakitamani kuona miradi ya maendeleo na uwekezaji na ameridhia ombi hilo kwa vitendo.

Amesema tayari wadau wengi wamejitokeza na kuonyesha utayari wa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho ikiwamo bwalo la watoto litakalokuwa sehemu ya kituo hicho cha vipaji.

Pia amesema wanamichezo mashuhuri nchini na nje ya nchi wakiwamo makocha wa zamani wa Klabu ya Yanga, Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi, wachezaji Skudu Makudubela,bAziz Ki, Feisal Salum “Fei Toto”, Aisha Masaka, Waziri Jr, Zidane, Boniface Pawasa, Edna Lema na Dickson Job wameonyesha utayari wa kumuunga mkono katika kuendeleza michezo na vipaji kwa vijana wa jimbo hilo.

Katika hatua nyingine, amewahakikishia wananchi kuwa atakamilisha upimaji wa ardhi ili kila mkazi wa Ipala, Sokoine na Mwinyi aweze kumiliki hati miliki kwa urahisi.

Amesema atahakikisha kupitia kliniki ya ardhi ofisi ya Idara ya Ardhi ya Jiji itahamishiwa eneo hilo kwa ajili ya kumaliza kabisa changamoto za muda mrefu za ardhi zinazowakabili wananchi.

Kuhusu changamoto ya maji, amesema atahakikisha tatizo hilo linakwisha kwa kuchimba visima vyenye uwezo wa kuhudumia eneo lote la Ipala, akibainisha kuwa changamoto ya maji itabaki kuwa historia baada ya miradi hiyo kukamilika.

Amesema zahanati ya sasa imekuwa ndogo kutokana na ongezeko la watu katika kata hiyo na Novemba, mwaka huu baada ya kuapishwa, ataanza ujenzi wa kituo kipya cha afya kitakachotoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi wa Ipala na maeneo jirani.