MVUTANO wa kibiashara kati ya Marekani na China umechukua sura mpya baada ya mataifa hayo mawili kuanza kutozana ada za bandari kwa kampuni za usafirishaji baharini.
Marekani na China zimeanza rasmi kutoza ada za bandari kwa kampuni za usafirishaji majini zinazoendesha meli kati ya nchi hizo mbili, hatua ambayo wachambuzi wanaiona kama ukurasa mpya wa vita vya kibiashara.
Ada hizo mpya zinahusu meli zinazobeba bidhaa mbalimbali kutoka petroli hadi vinyago vya msimu wa likizo, na zimezua taharuki katika sekta ya usafirishaji wa kimataifa.
China ilisema ada hizo zitalenga meli zinazomilikiwa, kuendeshwa au kujengwa na Marekani, huku ikizipatia msamaha meli zilizojengwa katika viwanda vya China. Wakati huo huo, serikali ya Rais Donald Trump imeanza kutoza ada zinazofanana kwa meli zinazohusiana na China, ikisema lengo ni “kuimarisha uwezo wa Marekani katika sekta ya ujenzi wa meli na kupunguza utegemezi kwa Beijing.”
Wataalamu wa biashara walisema hatua hizo za kulipizana zinaweza kusababisha ongezeko la gharama za usafiri na kuchelewesha mizigo duniani.
Ripoti ya kampuni ya Xclusiv Shipbrokers yenye makao yake Athens imeonya kwamba “ushindani huu wa ada za bandari unaweza kupotosha mtiririko wa mizigo ya baharini na kuathiri masoko ya mafuta na bidhaa za kilimo.”
Wizara ya Biashara ya China imesema inachukulia hatua za Marekani kama uchokozi wa wazi, lakini imeacha mlango wazi wa mazungumzo. “Ikiwa Marekani itachagua mazungumzo, China ipo tayari kushirikiana; lakini ikichagua mgogoro, China iko tayari kupambana hadi mwisho,” imesema wizara hiyo kupitia taarifa yake.
Wachambuzi wanaonya kuwa iwapo hatua hizi hazitadhibitiwa, zinaweza kufungua pazia jipya la vita vya kiuchumi kati ya nguvu mbili kubwa za dunia.
