Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida

Wakazi wa Kijiji cha Miganga wilayani Mkalama, mkoani Singida, wameishukuru Serikali kwa neema ya miradi ya uchimbaji wa visima vya Umwagiliaji na kuahidi kulinda miundombinu hiyo kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Wamesema kwa sasa wana matumaini mapya ya kuongeza uzalishaji baada ya Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC ) kuanzisha upya mradi wa kilimo cha Umwagiliaji wa visima uliokuwa umesimama kwa zaidi ya miaka 40.

Aidha mmoja wa wakazi hao Abdalah Kitundu, amesema ujio wa miradi hiyo ya visima ni neema kubwa baada ya changamoto ndefu ya ukame.

Naye Athuman Mazengo,amesisitiza kuwa, ujio wa mradi huo ni kicheko na matumaini kwa wanakijiji.

“Mradi huu wa awali uliporomoka miongo minne iliyopita na kusababisha wakulima wengi kushindwa kufanya kilimo cha umwagiliaji.

“ Baada ya kilio cha muda mrefu kutoka kwa wananchi, Serikali imetuitika tumepata visima kwa ajili ya Umwagiliaji tunafuraha sana,”amesema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho Abdalah Pyuza, ameeleza furaha yao akisema mradi huo utawasaidia kurudi kwenye kilimo cha kisasa na uhakika na kuongeza kipato cha familia zao na Taifa kwa ujumla.

Naye Maria Musa na Rehema Stephano
wameongeza kuwa, mradi huo utasaidia kuokoa maisha ya watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa kwenda kutafuta kazi na badala yake watajikita katika uzalishaji katika kilimo biashara.

Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoani Singida Emanuel Charo amesema Tume inaendelea kutekeleza miradi ya uchimbaji wa mabwawa na visima katika awamu mbalimbali ikiwemo uchimbaji wa visima.

Amesema katika awamu ya kwanza Tume itachimba visima 30 , mkoani humo ambapo 25 vimekamilika na matarajio visima hivyo vitamwagilia ukubwa wa mashamba ya hekta 1,200.

“Awamu ya pili itahusisha ufungaji pampu katika kila kisima cha Umwagiliaji kilichopo na vilevile kutawekwa matanki lengo ni kumrahisishia mkulima katika kumwagilia.Pia mradi huu utachochea upatikanaji wa ajira kwa vijana , kuongeza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja kwa kaya na Taifa sambamba kuongeza upatikanaji wa chakula na mboga mboga,”amesema.

Naye Afisa kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Oscar Mwilongo, amesisistiza kuwa visima hivyo vitasaidia kufufua shughuli za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wa eneo hilo.