Mwili wa Raila Amollo Odinga unatarajiwa kuwasili saa tatu na nusu asubuhi ya leo kutoka India, ambako alikuwa anapata matibabu kabla ya kupatwa na mauti.
Familia yake imefichua kwamba ndani ya wosia wake, aliandika kuwa azikwe ndani ya saa 72.
Chanzo cha familia kilisema Rais William Ruto alifahamishwa kuhusu hilo punde tu alipowasili nyumbani kwa Raila Odinga huko Karen.
“Mzee aliweka katika Wosia wake kwamba azikwe ndani ya saa 72; Rais ameambiwa shughuli ya mazishi ziendane na ratiba hiyo,” chanzo cha familia kiliongeza.
Kufuatia hilo, Raila Odinga atazikwa Jumapili, Oktoba 19, 2025 katika makaburi ya familia huko Kango Ka Jaramogi, Nyamira, Bondo, kando ya kaburi la marehemu babake Jaramogi na mwanawe Fidel.
Mwili wa Odinga utakapofika, utapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee kuandaliwa kabla ya kuendelea na ratiba jinsi ilivyopangwa.
